KUKOSA hamu ya ngono ni tatizo ambalo wengi huona aibu kulizungumzia ingawa ni kitu kinachowanyima raha wanawake wengi.
Inakadiriwa kuwa asilimia 40 ya wanawake hupatwa na tatizo hili katika maisha yao, hata hivyo tatizo hili huwapata zaidi wanawake wenye umri kati ya miaka 45 na 65. Wataalamu wengi wa afya huwaambia wanawake wenye tatizo hili kuwa wana matatizo ya homoni. Kuwa na homoni za kutosha katika mwili ni muhimu kwa tendo la ndoa.
Homoni iitwayo istrojeni huhamasisha damu kwenda kwenye uke na kusaidia kulainisha uke wakati homoni iitwayo testosteronihuchochea hamu ya ngono.
Hata hivyo, hamu ya ngono kwa wanawake ni kitu chenye utata mwingi kwa maana msongo wa mawazo, mkazo, afya yake na uhusiano uliopo huchangia kuwa na hamu au kutokuwa na hamu ya tendo la ndoa.
Wanawake wengi mwanzo wanakuwa wanafanya ngono mara 5 kwa wiki na baadaye hamu hupotea na kuanza kufanya ngono mara moja kwa mwezi, tena kwa kujilazimisha. Tatizo hili linaweza kuanza kwa mwanamke kukosa msisimko (raha ya tendo), kutofikia kileleni au kufika kileleni na kushindwa kuendelea na tendo la ndoa baada ya mzunguko mmoja, yaani goli moja na mchezo umekwisha.
Wanawake gani wako katika Hatari ya Kupatwa na tatizo hili?
Wanawake ambao waliwahi kupatwa na tatizo la kupungua hamu ya kujamiana hapo mwanzo wanaweza kupatwa na tatizo hili tena.
Wale ambao wamefanyiwa upasuaji wa kuondoa mayai yao ya uzazi kutokana na sababu mbalimbali kama magonjwa au uzazi wa mpango.
Wanawake ambao wamefika umri wa kukoma hedhi mara nyingi huanzia kati ya miaka 45 na 55 ingawa kuna wachache huanza kabla ya umri huo.
Matatizo ya homoni siyo chanzo pekee cha kukosa hamu ya ngono. Sababu nyingine ni pamoja na zifuatazo.
Mzunguko Mbovu wa Hedhi au Kukuosa kabisa Hedhi.
Ikiwa mwanamke ana mzunguko wa kati ya siku 24 hadi 34 ni dalili kuwa ovari na homini zake zinafanya kazi vizuri. Mzunguko mbovu wa hedhi au kutopata kabisa hedhi huwa ni ishara kuwa homoni za mwanake haziko vizuri.
Kukosa hedhi kwa zaidi ya miezi 6 ni ishara hakuna uwiano mzuri wa homoni ya istrojeni. Tatizo hili linaweza kuathiri tendo la ndoa na ni vyema kumuona daktari kwa msaada zaidi.
Kukoma Hedhi (Menopause).
Baada ya hedhi kukoma, ovari za mwanamke huacha kutengeneza homoni, hivyo kiasi cha homoni ya istrojeni na testosteronehupungua sana na wakati mwingine huisha kabisa.
Wanawake wengi katika kipindi hiki hupatwa na shida ya uke kukauka (kukosa ute wa kutosha) na kupungua hamu ya tendo la ndoa. Kupungua kwa homoni ya istrojeni husababisha nyama ya uke kuwa nyembamba na kukauka hivyo kusababisha maumivu wakati wa tendo la ndoa.
Ikiwa tendo la ndoa litasababisha maumivu kwa mwanamke hatataka kufanya tendo hilo mara kwa mara na jinsi anavyofanya mara chache ndivyo tatizo linavyokua.
Wakati mwingine tatizo la uke kukauka linaweza kutatuliwa kwa kupaka mafuta ya kulainisha uke au mafuta ya nazi.
Matumizi ya virutubishi vya homoni ya testosterone yanaweza kusaidia na kuongeza hamu ya tendo la ndoa kwa wanawake waliokaribia kukoma hedhi na wale waliokoma hedhi, ingawa virutubisho hivi huweza kusababisha chunusi, kuota nywele mwilini na huongeza kiwango cha lehemu (cholesterol) kitu ambacho kinaweza kusababisha matatizo ya moyo.
Matatizo ya Kihisia.
Kuwa na wasiwasi, msongo wa mawazo na mikazo katika maisha ambayo huchangiwa na matatizo ya uchumi, matatizo katika mahusiano kama ugomvi, kutoelewana, kutoaminiana huathiri mwili na kufanya homoni muhimu kwa ajili ya tendo la ndoa kutotengenezwa kwa kiwango cha kutosha.
Pia, mzunguko wa damu katika tupu ya mwanamke hupungua na hivyo kusababisha maumivu wakati wa kujamiana.
Historia ya kubakwa, au kupata maumivu wakati wa kujamiana hapo awali kutokana na mwanamke kutokuwa tayari kujamiana au kutotayarishwa vyema kabla ya kujamiana husababisha uke kuwa mdogo kuruhusu uume kupita, tatizo linalojulikana kitaalam kama vaginismus.
Matumizi ya Vilevi Mbalimbali.
Matumizi ya madawa ya kulevya na unywaji pombe kupita kiasi hupunguza hamu ya tendo la ndoa, ingawa kuna baadhi ya watu huamini unywaji pombe kali huongeza hamu ya kujamiana au kupunguza uzito.
Pombe kali au kilevi cha aina yoyote vikitumiwa kupita kiasi hupunguza hamu ya kujamiana na pombe huongeza uzito na kusababisha utapiamlo hasa kitambi.
Maradhi Mbalimbali.
Magonjwa kama kisukari, magonjwa ya mifupa (arthritis), magonjwa ya moyo, saratani ya aina yoyote ile, matatizo ya kupungua kwa homoni ya tezi la koo (hypothyroidism) ambayo hutokea sana kwa wanawake kuliko wanaume husababisha kupungua hamu ya tendo la ndoa vilevile madhara ya dawa mbalimbali kama dawa za kushusha shinikizo la damu, dawa za saratani nk.
Ujauzito, Kujifungua na Kunyonyesha Mtoto.
Mwanamke anaweza kukosa hamu ya tendo la ndoa kutokana na mabadiliko katika mfumo wa homoni au vichocheo wakati wa ujauzito pia kutokana na mabadiliko ya maumbile ya wanawake wakati huo na kufanya mwanamke kutojiamini kufanya tendo la ndoa.
Mwanamke akijifungua na kuanza kunyonyesha homoni yaprolactin huwa katika kiwango cha juu.
Homoni hii hufanya kazi ya kumfanya mtu kuridhika baada ya ngono/tendo la ndoa (kujamiana), hushirikiana na homoni/kichocheo nyingine iitwayo dopamine inayofanya mtu kufikia kilele wakati wa tendo la ndoa.
Hata hivyo, homoni ya prolactin inaweza kuongezeka wakati mtu amelala usingizi mzito hasa wakati wa alfajiri, baada ya kufanya mazoezi, kula, baada ya tendo la kujamiana, baada ya upasuaji mdogo na hata baada ya kupata degedege.
Sababu zingine za kuongezeka kiwango cha homoni hii ni kuwa na saratani katika ubongo.
Vidonge vya Uzazi wa Mpango.
Vidonge vingi vya uzazi wa mpango hugandisha homoni yatestosterone kwenye mwili na huweza kusababisha kupungua kwa hamu ya ngono kwa baadhi ya wanawake.
Ikiwa una hofu juu ya njia ya uzazi wa mpango yenye homoni ni vyema kuzungumza na daktari juu ya njia nyingine ya uzazi wa mpango isiyokuwa na homoni. Usiache tu kutumia vidonge vya uzazi wa mpango kwa kuhisi ndiyo sababu ya wewe kutopata hamu ya tendo la ndoa bila kuzungumza na mtaalamu wa afya.
Mambo Mengine!
Uharibifu wa neva inayohusika na kuongeza msisimko wakati wa kujamiana (pudendal nerve) wakati wa upasuaji wa kuondoa mfuko wa uzazi kwa mwanamke mwenye matatizo ya uzazi au katika mfuko wa kizazi.
Uchovu mwingi baada ya majukumu ya kulea mtoto/watoto, kazi na kumhudumia mume wake.
Matumizi ya vifaa vya kieletroniki kupita kiasi hasa uraibu wamitandao ya kijamii kama Facebook & Instagram, kupenda sana kuchat au kutumia intaneti kupita kiasi na hivyo kusababisha msisimko kupotea kati ya wenza wawili.
ASANTE SANA KUTEMBELEA BLOGU YETU....KARIBU TENA.
No comments:
Post a Comment