VIDONDA vya Kinywa ni michubuko inayotokea kwenye mdomo na ulimi. Vidonda hivi husababisha mhusika kupata maumivu kwa maana kinywa ni moja ya sehemu ya mwili yenye mishipa mingi ya fahamu na wakati mwingine vidonda katika kinywa husababisha kushindwa kuongea vizuri.
Ingawa vidonda hukufanya ujisikie vibaya, huwa vinapona vyenyewe ndani ya wiki moja au mbili. Vidonda vya Kinywa hutokea kwenye au ndani ya mashavu, midomo (lips), ulimi, kingo na kuta za meno pia huweza kusambaa mpaka kwenye koromeo ikiwa havitatibiwa kwa wakati.
Aina za Vidonda vya Kinywa
Vidonda vya mdomo huwa vya duara na hutokea ndani ya kinywa, kwenye ulimi na midomo. Vinaweza kuvimba na kuwa vyeupe, vyekundu au vya kijivu. Inawezekana kuwa na kidonda kimoja au zaidi wakati mmoja na kusambaa ndani ya kinywa.
Vidonda vya kinywa vinaweza kugawanywa katika aina mbalimbali kulingana na vigezo tofauti. Kwa kutumia kigezo cha ukubwa kuna aina kuu tatu za vidonda. 
Aina ya kwanza, ni kidonda kidogo kikiwa na kipenyo cha 1-10mm. Aina hii ya vidonda hujirudia kwa asilimia 80-85 na ndivyo huwapata sana watoto. Vidonda hivi hupona kati ya siku saba hadi kumi.
Aina ya pili, ni vidonda vikubwa. Hivi huwa na ukubwa wa kipenyo cha zaidi ya 10mm, huwa vinajirudia kwa siku kumi hadi 30 huku vikiacha kovu baada kupona.
Aina ya tatu ya vidonda, ni ile ambayo huota kwa wingi na kwa makundi. Vidonda hivi hujirudia kwa asilimia 5-10 na hupona kati ya siku saba hadi kumi.
Aina nyingine ya vidonda vya kinywa ni vidonda baridi (cold sores), huwa kama malengelenge kwenye midomo (lips). Vidonda hivi huwa na maumivu ya kuchoma choma na husababishwa na virusi aina ya herpes simplex.
Wakati Gani Unapaswa Kupata Msaada wa Kitabibu?
Vidonda mdomoni huwatokea watu wengi kwa kawaida na hupona bila ya matibabu ya daktari wa kinywa. Ikiwa vidonda vitatudumu zaidi ya wiki tatu, zungumza na daktari. Ikiwa vidonda vitauma na vitakufanya ushindwe kula, kunywa au kusukutua meno. Ikiwa vidonda vinajirudiarudia, au vidonda vinapokuwa na maumivu zaidi au vyekundu kitu kinachoweza kuashiria maambukizi ya bacteria.
Vidonda kwenye kinywa vinaweza kuwa moja ya dalili ya ugonjwa unaosababishwa na virusi unaoathiri mikono, miguu na mdomo. Ugonjwa huathiri zaidi watoto chini ya miaka 10 wakati mwingine huathiri hata watu wazima. 
Matibabu yanaweza kupunguza uvimbe na kuondoa wasiwasi. Vitu unavyoweza kufanya kuharakisha uponaji wa vidonda ni pamoja na kupaka dawa kwenye vidonda, kutumia mswaki laini kusukutua meno, ktumia dawa ya meno isiyo na sodium laryl sulphate ambayo inaweza kukereketa, kutotumia vyakula vyenye viungo vingi na chumvi nyingi.
Je, Vidonda hivi ni Saratani ya Kinywa?
Mara chache kidonda kwenye kinywa kilichokaa muda mrefu kinaweza kuwa ni dalili ya Saratani ya Kinywa. Vidonda vinavyosababishwa na Saratani ya Kinywa mara nyingi hutokea juu ya ulimi au chini ya ulimi ingawa vinaweza kutokea popote pale kwenye kinywa. 
Vitu vinavyoongeza hatari ya kupata Saratani ya Kinywa ni pamoja na uvutaji au utumiaji wa bidhaa za tumbaku, unywaji pombe sana na kuwa na maambukizi ya virusi vya human papilloma(HPV). 
Ni muhimu kuigundua saratani mapema iwezekanavyo, kwa maana ikigundulika mapema inaweza kutibika kirahisi. Kufanya uchunguzi wa kinywa kwa madaktari wa kinywa ni njia bora kuweza kugundua dalili za mwanzo za Saratani ya Kinywa.
Nini Husababisha Vidonda kwenye Kinywa?
Mara nyingi chanzo cha vidonda kwenye kinywa si cha moja kwa moja. Mara nyingi kidonda kimoja kwenye kinywa husababishwa na uharibifu wa utando laini ndani ya kinywa kwa mfano unapojing’ata kwa bahati mbaya au unapokula chakula kigumu.
Haijulikani wazi ni nini husababisha vidonda kwenye kinywa ambavyo hujirudia mara kwa mara, lakini vitu vinavyochochea ni pamoja na msongo, wasiwasi, mabadiliko ya homoni, mfano, baadhi ya wanawake hupatwa na vidonda mdomoni wanapokuwa kwenye siku zao, ulaji wa baadhi ya vyakula mfano vyenye viungo vingi, kahawa, nyanya na unga wa ngano.
Kutumia dawa ya meno yenye sodium lauryl sulphate na kuacha kuvuta sigara ghafla, wengi wanaoacha kuvuta sigara kwa mara ya kwanza wanaweza kupatwa na vidonda mdomoni. Chembe za urithi pia zinahusishwa na kupatwa na vidonda mdomoni, angalau asilimia 40 ya watu wanaopatwa na vidonda mdomoni wameripoti kurithi kutoka kwenye familia zao. 
Vidonda vya Kinywa wakati mwingine husababishwa na magonjwa yanayosababishwa na virusi kama tetekuwanga, magonjwa ya fangasi, magonjwa ya mfumo wa umeng’enyaji wa chakula (Crohn’s Disease, Coeliac Disease), ugonjwa wa kuvimba sehemu za maungio za mwili (Reactive Arthritis), ugonjwa wa kuvimba mishipa ya damu (Behcet’s Disease), kinga ya mwili kudhoofu kutokana na VVU au Lupus, upungufu wa vitamin B na madini chuma.
Pia, Vidonda vya Kinywa vinaweza kusababishwa na matumizi ya dawa mbalimbali kama za kutibu magonjwa mbalimbali mfano kupanda kwa shinikizo la damu na dawa za kutuliza maumivu mfano ibuprofen.
Ninawezaje Kuzuia Vidonda vya Kinywa?
Inaweza kuwa ngumu kuzuia Vidonda vya Kinywa kwa sababu mara nyingi husababishwa na vitu ambavyo huwezi kuvizuia mfano chembe za urithi na maradhi mbalimbali. Ingawa kufanya yafuatayo kunaweza kupunguza hatari ya kupata Vidonda vya Kinywa mfano kuepuka vyakula fulani kama vyenye viungo vingi, kahawa au chokoleti.
Epuka kula vyakula vya moto au baridi sana ikiwa una vidonda tayari kwa maana huchelewesha kupona kwa vidonda, kula matunda kwa wingi na mboga za majani ili kuongeza vitamin na madini chuma vitu vinavyoongeza kinga ya mwili, kutotafuna chingamu, kusukutua meno yako na mswaki laini, kutumia dawa ya meno isiyo na sodium lauryl sulphate, kupunguza msongo na wasiwasi

ASANTE SANA KUTEMBELEA  BLOGU YETU...KARIBU TENA.