HPV ni moja ya magonjwa yanayoenezwa kwa njia ya ngono, wanaume na wanawake wako katika hatari ya kuambukizwa ugonjwa huu. HPV ni kifupi cha neno Human Papilloma Virus,kundi la virusi lenye aina zaidi ya 150 ya virusi vinavyohusiana.
HPV ni kirusi kinachoweza kuambukiza kutoka mtu mwenye
maambukizi hadi kwa asiye na maambukizi kwa njia ya kugusana ngozi wakati wa
tendo la ndoa. Virusi hivi huvutiwa na ngozi na sehemu zenye unyevunyevu kama
kwenye uke, njia ya haja kubwa, kichwa cha uume, mdomo, koo na mapafu. Virusi
hivi hushindwa kusitawi kwenye sehemu zingine za mwili pia.
Virusi vya HPV vipo dunia nzima ingawa maambukizi mengi ya
HPV hayasababishi dalili, maambukizi ya HPV sehemu za siri yakiendelea kwa muda
mrefu husababisha saratani ya shingo ya kizazi.
Virusi vya HPV vinaweza pia kusababisha aina zingine za
saratani katikati ya makalio, saratani ya kichwa na shingo na chunjua za sehemu
za siri (Genital Warts) yaani sugu katika sehemu za siri kwa
jinsia zote.
Aina za 6 na 11 za virusi vya HPV husababisha sugu
sehemu za siri (genital warts) wakati saratani
mbalimbali husababishwa na aina za 16, 18, 31, 33, 45, 52 na 58 za virusi vya
HPV.
Mamilioni ya watu ulimwenguni pote huambukizwa virusi
hivyo ambavyo inasemekana ndio ugonjwa wa zinaa ambao huwapata watu wengi
zaidi. Pia, virusi hivyo ndivyo kisababishi kikuu cha saratani inayowaua
wanawake wengi katika nchi maskini.
Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), virusi
hivyo ndivyo kisababishi kikuu cha saratani ya shingo ya kizazi ambayo
inashikiria nafasi ya pili katika saratani zote zinazowaathiri wanawake duniani
kote.
Kila mwaka, mamia ya maelfu ya wanawake huchunguzwa na
kupatikana na virusi vya HPV na kila mwaka maelfu hufa kwa sababu ya saratani
ya shingo ya kizazi ambayo husababishwa na virusi hivyo.
Mwaka 2008, kulikuwa na kadirio la kesi mpya 529, 000 za
saratani ya shingo ya kizazi huku kukiwa na vifo 274, 000 kutokana na saratani
hiyo. Zaidi ya 85% ya vifo vinatokana na saratani ya shingo ya kizazi hutokea
nchi zinazoendelea, ambayo ni 13% ya saratani zote za wanawake.
Virusi vya HPV hufanya wanaume na wanawake wapatwe na
vipele vigumu, kutia ndani vipele vinavyotokea kwenye viungo vya uzazi. Kwa
kawaida, vipele hivyo havina kansa. Ingawa kuna aina za virusi vya HPV zaidi ya
150, ni chache sana kati yazo ambazo husababisha kansa.
Mtu hupata saratani ya shingo ya kizazi ikiwa tu aina
fulani ya virusi hivyo vinakaa kwa muda mrefu. Kwa upande mwingine,
maambukizo mengi ya virusi hivyo hupona yenyewe baada ya kushindwa nguvu na
mfumo wa kinga wa mwili.
Ni kina nani wanaweza
kuambukizwa?
Wale hasa wanaoweza kuambukizwa ni wanawake wanaoanza
kufanya ngono wakiwa na umri mdogo, wale walio na wapenzi wengi wanaume, au
wale wanaofanya ngono na mwanaume ambaye ana wapenzi wengi wanawake. Mara
nyingi, mwanamume asiye na dalili zozote zinazoonekana za ugonjwa huo ndiye
humwambukiza mwenzi wake.
Hata hivyo, katika visa fulani, wanawake walio safi
kiadili au wale ambao labda hawajawahi kufanya ngono huambukizwa virusi hivyo.
Kwa mfano, uchunguzi wa hivi karibuni unaonyesha kwamba mtoto anaweza
kuambukizwa virusi hivyo mama anapojifungua, au mtu anaweza kuambukizwa kwa
njia nyingine. Ugonjwa huo unaweza kujitokeza miaka mingi baada ya mtu
kuambukizwa.
Pia, kuna mambo kadhaa yanayofanya mtu awe katika hatari
kubwa ya kupata HPV, mfano kuwa na upungufu wa kinga mwilini kama wenye VVU,
kuwa na mikwaruzo/vidonda kwenye ngozi hasa sehemu za siri, kugusana na mtu
mwenye chunjua (warts). Jambo jingine ni umri
ambapo chunjua za kawaida hutokea kwa watoto, chunjua za sehemu za siri(Genital Warts) hutokea kwa waliobalehe na watu
wazima na chunjua za visigino (Plantar Warts)
hutokea kwa watu wazima ingawa huanza kwa vijana.
Jinsi ya kujua endapo
umeambukizwa
Dalili za ugonjwa huo hazijitokezi waziwazi. Ikiwa chunjua(warts) zinaonekana, mtaalamu wa afya anaweza
kutoa bainisho (diagnosis) la ugonjwa huu
baada ya kutazama kwa makini. Vipimo vya ziada vinaweza kufanyika ili
kutathmini kwa undani uwepo wa HPV. Hatua muhimu ni kufanyiwa uchunguzi
wa chembe za mlango wa tumbo la uzazi, yaani pap smear, au Papanicolaou Smear.
Ikumbukwe kuwa, uchunguzi huo ulipewa jina la daktari
Mgiriki, George N. Papanicolaou, ambaye alivumbua mbinu ya kutia chembe rangi
ili kuzichunguza.
Ili kufanya uchunguzi huo, daktari hutoa chembe chache za
mlango wa tumbo la uzazi na kuzipeleka kwenye maabara ili zichunguzwe. Uchunguzi
huo unaweza kuonyesha ikiwa mtu ameambukizwa, ana uvimbe, au ana chembe zisizo
za kawaida. Inaripotiwa kwamba uchunguzi wa pap smear umepunguza idadi ya watu
wanaopatwa na saratani ya shingo ya kizazi na vifo vinavyosababishwa na kansa
hiyo.
Ikiwa matokeo ya uchunguzi huo hayaridhishi, kifaa maalumu
chenye kamera hutumiwa kuchunguza sehemu iliyoathiriwa. Kwa kutumia kifaa
hicho, daktari anaweza kuona ikiwa kuna kidonda. Sehemu za tishu zilizoathiriwa
hukatwa na kufanyiwa uchunguzi, kisha matibabu huanza. Siku hizi, uchunguzi wa
hali ya juu sana, unaweza kufanywa kwenye maabara. Uchunguzi huo unaweza
kuonyesha vizuri zaidi ikiwa mtu ameambukizwa.
Nini matibabu na kinga?
Mara chache chunjua huisha zenyewe bila matibabu ingawa
kuna matibabu kadhaa yanayoweza kudhibiti maambukizo ya HPV. Wataalamu hutumia
dawa za kupaka. Baadhi ya dawa hizo huharibu chembe zenye virusi hivyo, na
wengine husaidia mfumo wa kinga kupambana na virusi hivyo. Matibabu mengine
hutia ndani kuondoa sehemu iliyoathiriwa kwa kutumia umeme, leza, au kwa
kuigandisha. Ni muhimu kuzungumza na daktari ili akusaidie kuchagua matibabu
kulingana na aina ya chunjua zinazokukabili.
Chanjo kuu mbili za HPV zinazotafutiwa soko nchi nyingi
duniani kote zina uwezo wa kuzuia maambukizi ya virusi vya aina ya 16 & 18
ambavyo kwa pamoja husababisha 70% ya kesi zote za saratani ya shingo ya kizazi
duniani kote. Chanjo moja inaweza kuzuia chunjua za katikati ya makalio na
sehemu za siri (anogenital warts) ambazo
husababishwa na HPV aina ya 6 & 11. Kundi kubwa linalolengwa kwa ajili ya
chanjo hizi ni wasichana waliobalehe duniani kote.
Walioambukizwa wanapaswa kujua ingawa chunjua (warts)
zinaweza kuondolewa au kuondoka zenyewe, kirusi cha HPV kinaweza kubaki kwenye
mwili wako na unaweza kuendelea kuwaambukiza wengine kwa maana hamna matibabu
yatakayotoa kirusi cha HPV ndani ya mwili wako.
Mtu anawezaje kuepuka
kuambukizwa?
Usifanye ngono kabla hujaolewa. Pia ili kuzuia saratani ya
shingo ya kizazi, ni lazima wenzi wawe waaminifu. Hata hivyo, ni muhimu kujua kuhusu
HPV kwa kuwa unaweza kuzuia usiambukizwe virusi hivyo. Isitoshe, hata kama
maambukizo hayo yanajitokeza na kuenea, bado unaweza kutibiwa.
Shirika la WHO linasema: 'Mara nyimgi saratani ya shingo
ya kizazi inaweza kutibiwa ikigunduliwa mapema.' Mbali na kujifunza kuhusu
maadili, wanawake wanapaswa kujua kuhusu ugonjwa huo na kuelewa umuhimu wa
kufanyiwa uchunguzi mbalimbali kwa ukawaida kama vile pap smear.
Uchunguzi huo unapaswa kufanyiwa mtu anapofikia umri wa
miaka 18 au anapoanza kufanya ngono. Kasoro yoyote ikigunduliwa, mwanamke
anaweza kutibiwa. Bado wanasayansi wanaendelea kutafuta njia rahisi na zenye
matokeo zaidi za kuchunguza virusi vya HPV. Pia, chanjo za kuzuia na kutibu
ugonjwa huo zinaendelea kutengenezwa.
ASANTE KUTEMBELEA BLOGU YETU...KARIBU TENA.
No comments:
Post a Comment