MSOMAJI wetu ameuliza kama kuna
vipimo vikubwa zaidi na dawa za kutibu tatizo la moyo kupanuka. Anadai mwanzo
alikuwa anapumua kwa shida akaenda hospitali, wakampiga picha ya X-Ray na
kumwambia moyo wake umepanuka na mapigo ya moyo wake hayaendi vizuri. Alipewa
dawa za mwezi mzima, katumia ila bado anapumua kwa shida.
Moyo
Kupanuka ni Nini?
Moyo ni ogani ya misuli
iliyopo kwa mwanadamu na wanyama, kazi yake kubwa ni kusambaza damu sehemu
mbalimbali za mwili. Damu inayosambazwa huupa mwili oksijeni, virutubisho na
kuondoa takamwili.
Moyo hupanuka ili
kukabiliana na tatizo la misuli ya moyo kuharibika. Moyo kupanuka kunaweza kusababishwa na vitu vingi sana,
ila sababu kuu zinazopelekea moyo kupanuka ni kupanda kwa shinikizo la damu (hypertension) na
ugonjwa wa mishipa ya moyo kuziba (coronary artery disease).
Sababu zingine zinatia
ndani, maambukizi ya virusi katika moyo, valvu za moyo zisizo za kawaida,
ujauzito hasa kukaribia na kujifungua, upungufu wa damu mwilini,
ugonjwa/matatizo ya tezi, ugonjwa wa figo, matumizi mabaya ya pombe na madawa
ya kulevya, maambukizi ya VVU, matatizo ya moyo ya kurithi.
Hata hivyo, kuna sababu
zingine za kupanuka moyo zisizojulikana moja kwa moja.
Moyo uliopanuka unaweza
kushindwa kusukuma damu vizuri na kusababisha kupungua kwa nguvu ya moyo
kusukuma damu (congestive heart failure).
Kukiwa na matibabu
mazuri tatizo la moyo kupanuka linaweza kupungua na mgonjwa kujisikia vizuri
ingawa linahitaji matibabu kipindi chote cha maisha ya mtu husika.
Kuna
Aina Ngapi za Moyo Kupanuka?
Ugonjwa wa misuli ya moyo (Cardiomyopathy) husababisha
misuli ya moyo kukakamaa na kufanya moyo kujaribu kusukuma damu kwa nguvu zaidi
kitu kinachoweza kusababisha moyo kupanuka. Ugonjwa huu umegawanyika katika
aina kuu mbili, ugonjwa wa misuli ya moyo kupanuka (dilated cardiomyopathy)
na ugonjwa wa misuli ya moyo kuwa minene (hypertrophic cardiomyopathy).
Ugonjwa wa misuli ya
moyo kupanuka (dilated cardiomyopathy)
hutokea pale kuta zote za moyo yaani ventrikali za kushoto na kulia zinapokuwa
nyembamba na kuvutika kusababisha moyo kuongezeka.
Wakati ugonjwa wa misuli
ya moyo kuwa minene (hypertrophic cardiomyopathy)
hutokea pale ukuta wa kushoto wa moyo, yaani ventrikali ya kushoto, inaponenepa
isivyo kawaida na kufanya moyo kupanuka. Kupanda kwa shinikizo la damu
husababisha kupanuka kwa ventrikali ya kushoto.
Dalili
za Moyo Kupanuka ni zipi?
Dalili za moyo kupanuka
zinatofautiana kati ya mtu na mtu. Baadhi ya watu wanaweza kuwa bila dalili
zozote, wengine dalili chache na wengine dalili nyingi hasa kushindwa kupumua
vizuri.
Dalili za moyo kupanuka
zinatia ndani kupumua kwa shida, miguu kuvimba, tumbo kuwa kubwa, kuongezeka
uzito, uchovu na moyo kwenda mbio.
Utabaini
Vipi Moyo Umepanuka?
Baada ya kuzungumza na
daktari jinsi unavyojisikia, daktari anaweza kubaini kupanuka kwa moyo wako kwa
kukufanyia uchunguzi wa mwili wako.
Hata hivyo, vipimo vingi
vinaweza kufanyika kuweza kuthibisha bainisho hilo. Vipimo hivyo ni kama echocardiography (ultrasound of the heart),
kipimo kinachopima ukubwa wa moyo, unene wa misuli ya moyo na uwezo wa moyo
kusukuma damu. Vipimo vingine ni X-Ray ya kifua, CT Scan, MRI na vipimo vya
damu kama kuangalia VVU, ugonjwa wa tezi na wingi wa damu.
Matibabu
ya Moyo Kupanuka ni yapi?
Matibabu ya moyo
kupanuka hukazia sana chanzo cha moyo kupanuka mfano ugonjwa wa mishipa ya moyo
kuziba (coronary artery disease),
kupanda kwa shinikizo la damu, matumizi ya pombe na madawa ya kulevya.
Mgonjwa atapewa dawa
zitakazo tibu dalili kama kuvimba miguu na kutibu chanzo cha tatizo la moyo
kupanuka.
Moyo kupanuka ni hali
ambayo inaweza kutibiwa kwa urahisi ikiwa itagundulika mapema, hivyo ni vyema
kutafuta msaada wa kitabibu ikiwa unapata dalili yoyote kati ya hizo hapo juu.
Matibabu ya moyo mkubwa
yanaweza kuhusisha matumizi ya dawa, kubadili mfumo wa maisha na wakati
mwingine upasuaji wa moyo.
Niishi
Jinsi Gani ikiwa Nina Tatizo la Moyo Kupanuka?
Kuna njia zinazoweza
kuiboresha hali yako ingawa haiwezi kutibika kabisa. Daktari wako anaweza
kupendekeza aina ya maisha unayopaswa kuishi ikiwa ni pamoja na kuacha kuvuta
sigara, kupunguza uzito ikiwa uzito wako hauendani na kimo chako, kupunguza
matumizi ya chumvi kwenye vyakula vyako, kudhibiti kisukari, kudhibiti kupanda
kwa shinikizo la damu, kufanya mazoezi yanayopendekezwa kwako, kutotumia pombe
au kahawa na kupumzika vya kutosha, mfano kulala masaa nane usiku
ASANTE SANA KUTEMBELEA
BLOGU HII...KARIBU TENA
No comments:
Post a Comment