Saturday, September 10, 2016
UGONJWA WA MACHO KUTOONA MBALI(MYOPIA).
Tatizo la kutokuwa na uwezo wa kuona vitu vilivyo mbali ni changamoto ya uonaji inayowasumbua watu wengi sana Tanzania na duniani kwa ujumla.
Changamoto hii hutambulika kwa mtu kushindwa kuona vitu vilivyo mbali. Watu hawa wanapoangalia mbali hushindwa kutambua taswira zilizo mbali.
Tatizo la kutokuwa na uwezo wa kutoona vitu vilivyo mbali hutokea pale macho au jicho linapokuwa kubwa au sehemu ya jicho inayoruhusu mwanga wenye taswira kuingia ndani ya jicho; yaani cornea, kuwa imekunjika kuliko kawaida hivyo kushindwa kuelekeza mwanga wenye taswira kutua kwenye eneo la nyuma la jicho linalohusika na kusafirisha kile kinachoonekana kwa ajili ya kutafsiriwa kwenye ubongo.
Hali hizi mbili husababisha mwanga wenye taswira unaoingia kwenye jicho kutoweza kufikia eneo la nyuma ya jicho yaani retina.
Hii husababisha retina kushindwa kupeleka taarifa zenye taswira kwenye ubongo na matokeo yake hushindwa kutafsiri taswira ambayo mtu anajaribu kuitazama. Matokeo yake ni wewe kushindwa kutambua unatazama nini.
Mpaka sasa sababu ya kwa nini watu wengine wanakuwa na macho makubwa, haijajulikana ila kuna hisia kuwa hali hii hutokana na vinasaba na ndiyo maana tatizo hili huoneakana zaidi kwenye familia zenye watu wenye tatizo hili.
Watu ambao kwenye familia kuna historia ya tatizo hili ndio wako hatarini kukumbwa na hali hii. Kama mzazi mmoja au wote wawili wana tatizo hili (na wanavaa miwani) basi kuna uwezekano wa karibu asilimia 95 kwa mmoja wa watoto kuwa na tatizo hilo pia.
Wengine ni watu wanaotumia muda mwingi sana kujisomea na wale wanaokosa muda wa kutoka nje na kupata fursa ya kuangalia mbali mara kwa mara.
Dalili za kutokuwa na uwezo wa kuona mbali ni kushindwa kutambua taswira halisi ya vitu vilivyo mbali, kufinya macho au kukunja sura mara unapotaka kuangalia mbali, kuumwa kichwa kutokana na kutumia nguvu nyingi kujaribu kutambua taswira ya vitu vilivyo mbali na kushindwa kuona nyakati za usiku.
Kwa watoto changamoto hii mara nyingi hutambulika tangu mtu mwenye tatizo hili akiwa mdogo kabisa kiumri au anaonekana akiwa amekunja uso au kufinya macho au anasogea karibu na runinga wakati anatazama au darasani mtoto anaonekana akisogea karibu na mwalimu.
Dalili ya tatizo hili kwa watoto pia ni kutofahamu kabisa yanayoendelea mbali na mahali alipo au kufikicha macho mara kwa mara.
Tatizo hili hugunduliwa kwa vipimo vya kawaida tu vya macho vinavyopatikana katika hospitali maalum za matibabu ya matatizo ya macho.
Vipimo hivi hupatikana kirahisi zaidi tukilinganisha na vipimo vya kupima tatizo la kutoona vitu vilivyo karibu.
Hata hivyo mtu yeyote mwenye matatizo ya macho anapaswa kwenda hospitali ili kuchunguzwa na kupatiwa matibabu sahihi. Mgonjwa yeyote wa macho anapaswa kuepuka kutumia miwani hata kama inaonekana kumsaidia kutatua tatizo hadi amepatiwa na mtaalamu hospitalini.
ASANTE SANA KUTEMBELEA BLOGU YETU....KARIBU TENA.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment