1. KUWASHWA sehemu za siri kunaweza kuwa dalili ya maradhi fulani kujumuisha maradhi ya uke kwa wanawake au muwasho na kuvimba kwa sehemu za siri za wanaume (jock itch). Bila kujali jinsia muwasho unaweza kusababishwa na ugonjwa wa ngozi, magonjwa ya zinaa au mzio (allery).

Kuwashwa makalioni hutokea pale ngozi inayozunguka njia ya haja kubwa inapokereketa ikiambatana na hamu ya kutaka kupakuna, muwasho huongezeka pale unapokaa na kukiwa na unyevunyevu. Aidha, sababu kuu za kuwashwa kwenye makalio ni kutojisafisha vizuri, kula vyakula vyenye viungo vingi sana, kuhara, vidonda kwenye njia ya haja kubwa, maambukizi ya fangasi, bawasiri (hemorrhoids), minyoo na kadhalika.
Watu wengi wakiwemo wasomaji wa TABIBU WA KWELI wamekuwa na tatizo la muwasho sehemu za siri unaosababishwa na kitu flani na huisha wenyewe baada ya kitu hicho kikiondolewa, vitu vingine vinavyosababisha muwasho huhitaji matibabu ya hali ya juu zaidi, ikiwa unawashwa kwa muda mrefu ni vyema kuzungumza na daktari.
Nini husababisha muwasho sehemu za siri za Mwanaume?
Kuwashwa uume au sehemu zingine za siri za mwanaume husababishwa na sababu zilezile zinazosababisha muwasho sehemu zingine za mwili. Maambukizi hasa ya magonjwa ya zinaa ndio chanzo kikuu cha kuwashwa uume. Sababu zingine ni maradhi ya fangasi, ugonjwa wa upele (scabies), kuwepo kwa chawa, mzio, maambukizi ya bakteria n.k
Nini hupelekea muwasho wa sehemu za siri kwa Mwanamke?
(i) Maambukizi ya Fangasi Ukeni (Vaginal Yeast Infection), Ni moja ya tatizo kwa wanawake linalosababishwa na fangasi waitwao Candida. Dalili kuu ni uwashwa ukeni, kuvimba na kutoa uchafu mweupe kama maziwa ukeni.
(ii) Ugonjwa wa kuvimba uke (Vulvovaginitis), Ni ugonjwa unaoathiri kwa kuvimbisha sehemu za nje za uke na uke wenyewe. Dalili kuu ni kuwashwa ukeni, mkojo kuuma na kukereketa wakati wa kukojoa na kutokwa na uchafu ukeni.
(iii) Kuvimba Uke baada ya hedhi kukoma (Postmenopausal Atrophic Vaginitis), Ni ugonjwa wa kuvimba kwa uke baada ya hedhi kukoma. Hali hii huongeza maambukizi ukeni na huweza kusababisha maumivu wakati wa tendo la ndoa.
(iv) Maambukizi ya Trikomonasi (Trichomonas Infection), Ni ugonjwa wa zinaa unaosababishwa na kimelea aitwaye Trichomonas vaginalis. Dalili kuu ni muwasho katika uke au uume na kutokwa na uchafu ukeni.
(v) Ugonjwa wa Minyoo (Pinworm Infection), Ni maambukizi ya minyoo wadogo sana wenye umbo la pini wanaoweza kuambukiza utumbo na kusambaa maeneo mbalimbali. Ugonjwa huu huwatokea sana watoto wa kati ya miaka 5 na 10.
(vi) Inflamesheni ya Urethra (Urethritis), Ni maambukizi kwenye urethra (ujia wa kutolea mkojo nje) yanasababisha kuvimba kwa urethra. Dalili kuu ni mkojo kuchoma, maumivu ya tumbo chini ya kitovu na kutokwa uchafu.
(vii) Genital Warts, Ni vivimbe vidogo vinavyotokea juu ya ngozi sehemu za siri. Ugonjwa unaoenezwa kwa njia ya kujamiana na unasababishwa na virusi viitavyo Human papillomavirus (HPV). Vivimbe vinaweza sababisha muwasho na maumivu.
(viii) Saratani ya sehemu ya nje ya Uke (Vulvar Cancer), Ni saratani ya sehemu ya nje ya uke inayoambatana na kuwashwa sehemu ya nje ya uke.
(ix) Ugonjwa wa Wasiwasi (Generalized Anxiety Disorder), Ni ugonjwa ambao unaotokana na hofu ya matukio fulani. Wakati mwingine husababisha kujikuna sehemu mbalimbali hata sehemu za siri.
(x) Ugonjwa wa Sjogren (Sjogren's Syndrome), Ni ugonjwa katika mfumo wa kinga ya mwili unaoathiri tezi zinazosaidia mwili kutengeneza unyevu nyevu kwenye macho na mdomo. Ugonjwa huu huathiri wanawake zaidi kuliko wanaume.
(xi) Kisukari, Ni ugonjwa sugu wa kimetaboliki unaosababishwa na kasoro katika utengenezaji wa Insulin au utendaji kazi wake. Kisukari kilichokomaa kinaweza sababisha maumivu ya tumbo, kichefuchefu, kizunguzungu na kuwashwa sehemu za siri.
Wanaume wanapaswa kufuata hatua zifuatazo ili kusaidia kuepuka kuwashwa sehemu za siri, Jambo la kwanza ni kwa mwanaume kuhakikisha kuwa anaosha vizuri uume na kwa wale ambao hawajatahiriwa wanapaswa kuosha kwa umakini zaidi hadi sehemu za ndani za govi.
Aidha, ziweke sehemu zako za siri kutia ndani makalio katika hali ya usafi na ukavu, kwa maana unyevunyevu unaweza sababisha maambukizi. Matumizi ya poda ya Cornstarch yanaruhusiwa hasa kipindi cha joto kali.
Hakikisha unavaa nguo isiyobana sana, iliyotengenezwa kwa vitu asilia kama pamba. Badili nguo ya ndani (chupi) angalau kila siku. Vaa kondomu kila unapofanya ngono na mwanamke usiyejua hali yake kiafya kiujumla.
Kwa Wanawake wanapaswa kufunya hata ili kuwasaidia kuepuka kuwashwa sehemu za siri
Baada ya kukojoa au kujisaidia osha sehemu zako za siri kuanzia mbele (ukeni) kwenda nyuma (makalio) ili kuzuia bakteria kutoka njia ya haja kubwani kuingia ukeni.
Epuka matumizi ya vitu vyenye kemikali kama marashi ya uke katika kusafisha uke kwa maana huharibu hali ya asidi ya uke na kuua bakteria wanaolinda uke na kufanya iwe vyepesi kushambuliwa na maradhi.
Hata hivyo, weka sehemu zako za siri katika usafi na ukavu, tumia sabuni kidogo katika kusafisha sehemu zako za siri na maji mengi. Kausha sehemu zako za siri kila baada ya kuoga au kuogelea na epuka kukaa na nguo mbichi kwa muda mrefu.
Vaa nguo isiyobana sana, iliyotengenezwa kwa pamba ili unyevunyevu usitokee na badili nguo za ndani kila baada ya masaa 24. Epuka ngono bila kuvaa mpira (kondomu) hasa ukiwa na hofu na mpenzi kuwa ana maradhi.
Ikiwa unaendelea kuwashwa tu hata baada ya kufuata njia hizo hapo juu ni jambo la busara kufika hospitali kwa ajili ya matibabu zaidi na ushauri wa kitiba

ASANTE SANA KUTEMBELEA BLOGU YETU....KARIBU TENA.