MAAMBUKIZI
sugu ya njia ya mkojo (chronic urinary tract infections – UTIs) ni
maambukizi kwenye njia ya mkojo ambayo hayatibiki kwa urahisi au yanajirudia
mara kwa mara, Tabibu wa Kweli inaripoti kwa kina.
Maambukizi
haya yanaweza kuendelea kuathiri njia ya mkojo hata baada ya kupata matibabu
sahihi au yanaweza kujirudia muda mfupi baada ya matibabu.
Njia
ya mkojo huunda mfumo wa mkojo ukiwa na ogani mbalimbali kama figo, ureta
(mirija inayobeba mkojo kutoka kwenye figo kwenda kwenye kibofu cha mkojo),
kibofu cha mkojo na urethra (mirija inayobeba mkojo kutoka kwenye kibofu cha
mkojo kutoa nje).
Maambukizi kwenye njia ya mkojo
yanaweza kutokea sehemu yoyote ya mfumo wa mkojo. Ikiwa maambukizi yataathiri
kibofu cha mkojo peke yake ni rahisi hali hii kutibika, isipokuwa maambukizi
yakisambaa mpaka kwenye figo, unaweza kuumwa zaidi na pengine kulazwa
hospitali.
Ingawa
maambukizi ya njia ya mkojo yanaweza kumpata yeyote, wakati wowote bila kujali
jinsia na umri, maambukizi haya hutokea sana kwa jinsia ya kike. Tafiti ya National Institute of Diabetes
and Digestive and Kidney Diseases (NIDDK) inakadiria
kila wanawake watano kuna mmoja anasumbuliwa na maambukizi ya njia ya mkojo
yanayojirudia mara kwa mara.
Nini Huongeza Hatari ya Maambukizi Sugu ya Njia ya Mkojo?
Maumbile:
Maambukizi sugu ya njia ya mkojo huwapata sana jinsia ya kike kutokana na
maumbile yao.
Kwanza,
urethra ipo karibu sana na puru (rectum) kwa wanawake kitu
kinachorahisisha bacteria kutoka kwenye puru kuingia kwenye urethra hasa
ukichamba/kutawadha kwa kurudisha mkono kutoka nyuma kwenda mbele. Hii ni moja
ya sababu kubwa ya watoto wadogo wa kike kupata maambukizi ya njia ya mkojo kwa
kuwa bado hawajajifunza jinsi ya kuchamba vizuri.
Pili,
urethra ya mwanamke ni fupi zaidi ikilinganishwa na ya mwanaume. Hii ina maana
bacteria wana umbali mfupi zaidi wa kusafiri kufika kwenye kibofu cha mkojo
ambapo wanaweza kuzaliana na kuongezeka kiurahisi na kusababisha maambukizi.
Aina ya Maisha: Kuna
aina ya maisha ambayo yanaweza kukufanya uwe kwenye hatari zaidi ya kupata
maambukizi sugu ya njia ya mkojo kwa urahisi. Kwa mfano kutumia diaphragm
(mpira laini maalum unaowekwa ukeni wenye kizibo cha kuzuia mbegu za mwanamume
kupenya ili kukutana na yai la mwanamke) inaweza kusukuma juu urethra na
kufanya iwe vigumu kutoa mkojo wote baada ya kukojoa. Mkojo unaobaki kwenye
kibofu huongeza uwezekano wa bacteria kuzaliana na kusababisha maambukizi.
Mfano
mwingine ni pale mwanamke anapobadili muundo wa kinga ndani ya uke wake kwa
kutumia vitu vyenye kemikali kuosha uke wake, zinazoua bacteria walinzi wa
kwenye uke, kama sabuni, marashi au viua shahawa (spermicides). Pia, kunywa dawa za
kuua bacteria mwilini huweza kuua bacteria walinzi kwenye uke. Hii inaweza
kuongeza hatari ya kupata maambukizi sugu ya njia ya mkojo.
Kukoma hedhi: Kukoma
hedhi husababisha mabadiliko ya homoni, ambayo mwisho husababisha kubadilika
kwa hali ya bacteria walinzi ndani ya uke hivyo kufanya wafe kwa wingi na uke
kukosa ulinzi na kufanya iwe rahisi kupata maambukizi ya njia ya mkojo mara kwa
mara.
Aina za Maambukizi Sugu ya Njia ya Mkojo ni zipi?
Maambukizi
ya njia ya mkojo husababishwa na bacteria. Mara nyingi bacteria huingia mfumo
wa mkojo kupitia urethra na kisha huzaliana na kuongezeka zaidi kwenye kibofu
cha mkojo. Ili kuelewa zaidi maambukizi haya jinsi yanavyotokea ni vizuri
kugawanya maambukizi katika kibofu cha mkojo na maambukizi katika urethra.
Maambukizi
katika kibofu cha mkojo (Cystitis) mara nyingi husababishwa
na bacteria waitwao Escherichia coli. E.coli ni
aina ya bacteria wanaoishi kwenye utumbo wa watu na wanyama wenye afya nzuri.
Bakteria hawa wakiwa mahala pao hawana madhara, isipokuwa wakipata upenyo wa
kutoka huenda njia ya mkojo na kusababisha maambukizi.
Mara
nyingi hutokea pale mabaki ya kinyesi yasiyoonekana yanapoingia njia ya mkojo.
Hii inaweza kutokea wakati wa kufanya ngono mfano mwanaume anapoingiza uume
mbele na nyuma (njia ya haja kubwa). Kushiriki ngono ya matakoni kunaongeza
hatari ya kupata maambukizi katika njia ya mkojo. Maambukizi pia yanaweza
kutokea wakati wa kujitawadha unapopeleka mabaki ya kinyesi mbele.
Maambukizi
katika urethra (Urethritis) yanaweza kusababishwa
na bacteria kama E.coli, lakini pia yanaweza
kusababishwa na magonjwa/maambikizi ya njia ya ngono (STI) kama pangusa,
kisonono au klamidia. Hata hivyo, magonjwa/maambukizi ya njia ya ngono
husababisha mara chache sana maambukizi ya njia ya mkojo.
Dalili za Maambukizi Sugu ya Njia ya Mkojo ni zipi?
Kukojoa
mara kwa mara, mkojo uliochanganyika na damu au mkojo mzito sana, kuhisi mkojo
kuchoma au maumivu wakati wa kukojoa, maumivu kwenye figo yaani chini ya mgongo
au chini ya mbavu, maumivu chini ya kitovu au kwenye kibofu cha mkojo.
Ikiwa
maambukizi yatasambaa hadi kwenye figo, yanaweza kusababisha kichefuchefu,
kutapika, baridi, homa kali (zaidi ya nyuzi za Fahrenheit 101 au nyuzi za
Centigrade 38.3), uchovu na kuchanganyikiwa.
Hali ikiwa Mbaya Kiasi Gani Ndio Nimuone Daktari?
Dalili
za maambukizi ya njia ya mkojo zinaweza zisiwe kali mwanzoni, isipokuwa baadaye
zikawa kali na kukufanya ujisikie vibaya. Ikiwa dalili zitakuwepo kwa zaidi ya
siku 5 ni vyema ukamuona daktari. Pia, muone daktari haraka ikiwa mwili
utachemka sana, ikiwa una mimba au kisukari.
Ikiwa
una maambukizi sugu ya njia ya mkojo hii ina maana ulikuwa na maambukizi ya
njia ya mkojo yaliyokuwa hayajatibiwa. Madaktari huwatuma wateja wao maabara
kwa ajili ya vipimo zaidi kubaini ni maambukizi ya aina gani. Wataalamu wa
maabara huangalia mkojo kupitia hadubini ili kuona bakteria wanaosababisha
maambukizi.
Kuotesha
mkojo (urine culture test) ni kipimo
kinachoweza kufanywa na wataalamu wa maabara ili kubaini aina mahususi ya
bacteria anasababisha maambukizi kwa ajili ya kurahisisha uchaguzi wa dawa kwa
daktari kulingana na bakteria. Kipimo hiki huchukua siku moja mpaka tatu.
Ikiwa
daktari atahisi kuna uharibifu wa figo kutokana na maambukizi atapendekeza
vipimo zaidi vya figo kama x-ray na ultrasound. Kama una maambukizi
yanayojirudia mara kwa mara daktari anaweza kufanya kipimo cha cystoscopy (kipimo
kinachohusisha mpira mrefu wenye lenzi mwishoni unaotumika kuangalia urethra na
kibofu cha mkojo). Daktari anaweza kuangalia pia tofauti za kimaumbile
alizonazo mwanamke zinazo sababisha kujirudia kwa maambukizi.
Nini Madhara ya Muda Mrefu ya Maambukizi Sugu ya Njia ya Mkojo?
Maambukizi
sugu ya njia ya mkojo yanaweza kusababisha maambukizi kwenye figo, ugonjwa wa
figo, kuharibika kwa figo hasa kwa watoto wadogo, kusambaa kwa bakteria kwenye
damu (septicaemia) na kuongezeka hatari
ya kuzaa watoto njiti kwa wajawazito.
Ninawezaje Kujikinga na Maambukizi Sugu ya Njia ya Mkojo?
Kojoa
mara nyingi uwezavyo muda wowote unapojihisi kukojoa. Wakati wa kuchamba,
safisha kwa kupeleka nyuma uchafu. Kunywa maji mengi kusafisha bakteria kwenye
njia ya mkojo kila mara unapokojoa, vaa chupi iliyoundwa kwa pamba, epuka kuvaa
nguo za ndani zinazobana sana. Epuka kutumi diaphragm kama njia ya uzazi wa
mpango
Tumia
mafuta ya kulainisha wakati wa tendo la ndoa ikiwa inawezekana ili kuondoa
michubuko isiyo ya lazima yenye kufanya upenyo wa bakteria na pia epuka kuoga
ndani ya mapovu mengi kwa kuwa kemikali zilizopo kwenye sabuni huingia kwenye
uke na kuua bakteria walinzi hivyo kufanya iwe rahisi kupata maambukizi. Ikiwa
haujatahiriwa osha vizuri uume wako mara kwa mara.
ASANTE
SANA KUTEMBELEA BLOGU YETU...KARIBU TENA.
No comments:
Post a Comment