Yapo madai kwamba wanaume wengi huwa ni wabishi wanaposhauriwa kuhudhuria vituo vya kutolea huduma za afya kwa ajili ya uchunguzi wa afya zao pamoja na ukweli kuwa uchunguzi wa afya mara kwa mara ndiyo njia sahihi ya kujikinga na maradhi mbalimbali kabla hayajafikia hatua ya kuhatarisha afya zao.
Kupima afya mara kwa mara ni muhimu kwa wanaume, hata kama hawana dalili zozote za magonjwa. Madaktari bingwa wa magonjwa ya tiba (Physicians) wanapendekeza wanaume kufanya uchunguzi wa afya zao walau mara moja kwa mwaka.
Hata hivyo, kama mtu ana viashiria hatarishi vya kuwa magonjwa sugu kama vile kisukari, anashauriwa kupima mara kwa mara afya yake. Kuna mambo ambayo ni muhimu kufanyiwa uchunguzi kwa mwanaume katika umri wowote na mengine ni muhimu zaidi katika umri mkubwa.
Mara nyingi, madaktari huunganisha maelezo yanayotolewa na mtu kutokana na dalili anazohisi mwilini mwake, historia ya maradhi yaliyowahi kumsumbua, uchunguzi wa mwili pamoja na kufanyiwa vipimo ili kugundua maradhi gani hasa yanamkabili.
Kwa hiyo, ni muhimu kwa mwanaume kumwambia daktari wake kuhusu vipimo anavyotaka afanyiwe, kwa kuwa mara nyingi vipimo hutegemea umri wa mtu, historia ya matatizo ya afya katika familia, mtindo wa maisha anaoishi kwa mfano vyakula anavyopendelea, aina ya kazi aifanyayo pamoja na unywaji pombe na uvutaji tumbaku.
Baadhi ya vipimo anavyopaswa kufanyiwa mwanaume ni pamoja na Tezi dume, shinikizo la damu, moyo, figo, kiharusi (stroke), kisukari, macho, kinywa, saratani kwa kutumia kipimo cha Colonoscopy, kiasi cha kolesteroli au lehemu mwilini, uzito na kimo. Shinikizo la damu linapaswa kupimwa kila anapofika hospitali kwa ajili ya kupata matibabu. Aidha, wakati mwingine saratani ya utumbo mpana huhitaji vifaa maalumu kwa ajili ya vipimo.
Vipimo vikubwa zaidi vya afya ya mwili mara nyingi huhitaji mgonjwa kukaa hospitali hadi usiku mnene. Vipimo hivyo hufanyika kwenye mwili wote ili kuhakikisha kila tatizo lililopo linajulikana.
Inashauriwa kwamba kabla ya mtu kufanyiwa vipimo, anatakiwa asile vyakula vizito kama vile ugali, saa 24 kabla ya muda wa kufanyiwa vipimo hivyo. Katika baadhi ya maeneo, kipimo cha X=Ray hutumika, kama vile kifua, vipimo vya mkojo, vipimo vya kinyesi, vipimo vya damu na vingine vingi tu.
Kwa mwanaume mwenye matatizo ya moyo, figo au kiharusi, anashauriwa kuhakikisha kwamba shinikizo la damu linakuwa la chini zaidi muda wote.
Wakati mwingine ugonjwa wa shinikizo la damu huendelea kupanda kadri umri wa mtu unavyoongezeka kwa sababu mishipa ya damu huwa inaongeza ugumu kulingana na umri unavyoongezeka. Shinikizo la juu la damu si nzuri kwa afya kwa kuwa linaongeza hatari ya kupata kiharusi, mshtuko wa moyo (heart attack), moyo kushindwa kufanya kazi (heart failure), ugonjwa wa figo na kifo cha mapema.
Kutokana na mfumo wa sasa wa maisha na vyakula tunavyokula, uchunguzi wa kiafya kwa mwanaume unapaswa uhusishe kipimo cha kubaini kiwango cha kolesteroli. Kuwa na kiwango kikubwa cha kolesteroli, maana yake ni kuwa na mafuta mengi kwenye damu kitu kinachoweza kusababisha hatari ya kupatwa na magonjwa ya moyo.
Aidha, mwanaume anapaswa kuwa na uzito unaofaa kiafya na kufanya mazoezi ya mwili. Njia sahihi ya kujua kama uzito na kimo viko sawa kiafya, ni kupata kipimo cha kupima Uwiano wa Uzito na Kimo (Body Mass Index-BMI).
Kikokotozi cha BMI mara nyingi hutumika kupata majibu sahihi. Kwa kawaida, BMI iliyo chini ya 18.5, inaashiria upungufu wa uzito, na kwa hiyo hapo kuna tatizo la kiafya. BMI ikiwa kati ya 18.5 na 25, huashiria afya njema. Hata hivyo, mtu mwenye BMI 30 na kuendelea huyo atakuwa na uzito kupita kiasi, kwa maana ya kitambi, hali ambayo ni tatizo pia.
Wanaume wenye umri wa miaka 50 na kuendelea, wanapaswa kufanyiwa vipimo vya Tezi dume. Kipimo hiki huweza kufanyika kwa kuingizwa vidole kwenye njia ya haja kubwa ili kubaini ukubwa wa Tezi dume. Kama imebainika kuwa Tezi dume ni kubwa, basi hiyo inaweza kuashiria ugonjwa wa saratani.
Aidha, Tezi dume huweza kuchunguzwa kwa kutumia kipimo ambacho kitaalam kinaitwa Prostate Specific Antigen (PSA). Hiki ni kipimo cha damu kinachosaidia kugundua saratani ya Tezi dume. Mwanaume anapaswa pia kufanyiwa uchunguzi wa utumbo mpana na njia ya haja kubwa (puru) ili kubaini kama kuna saratani ya utumbo mpana. Ugonjwa huo mara nyingi hutokea pindi unapojitokeza uvimbe usio wa kawaida kwenye utumbo mpana au njia ya haja kubwa.
Vipimo vya kolonoskopi vinaweza kugundua uvimbe mdogo mapema na kuruhusu daktari kuweza kuuondoa kwa upasuaji kabla haujakuwa Saratani. Matibabu ya Saratani hufanikiwa yakiwa katika hatua za mwanzo kabisa. Kutoa kinyesi kilichochanganyikana na damu inaweza kuwa dalili ya mwanzo ya Saratani ya utumbo mpana, hivyo kinyesi kinaweza kupimwa kugundua kama kuna Saratani hiyo.
Kama mtu ana umri wa chini ya miaka 40, anaweza kufanyiwa kipimo cha korodani. Kipimo hiki hufanywa kwa mteja kugeuza kichwa chini na kukohoa, huku daktari wake akiwa ameshika korodani ili kubaini kama kuna Henia. Ni muhimu pia kwa wanaume kufanya vipimo vya macho ili kuchunguza matatizo fulani ya macho. Vipimo hivyo vinaweza kuhusu uonaji na afya ya macho. Kufanyiwa vipimo vya macho kunaweza kugundua matatizo ya macho kama vile Glaukoma, Mtoto wa jicho (Cataract) na Age-Related Macular Degeneration (AMD).
Lakini pia ni muhimu kwa wanaume kufanya uchunguzi wa kinywa, kwa maana kukagua meno, fizi, ulimi na limfu za shingo. Inashauriwa kufanya uchunguzi wa kinywa kila baada ya miezi sita ili kumfanya mtu awe na kinywa chenye afya bora. Kipimo cha X-Ray wakati mwingine kinaweza kutumika katika uchunguzi wa kinywa, hasa kwenye meno.
Wataalam wa afya wanashauri mtu kujenga mazoea ya kufanya uchunguzi wa kiafya kwa kuwa kunasaidia kugundua maradhi mapema na kupata matibabu stahili kabla maradhi husika hayajaathiri mwili.
Kwa kadri ya makala haya ya TABIBU WA KWELI kuwa na afya njema kunamfanya mtu aweze kufikia malengo yake ya kiuchumi, kisiasa, kijamii na kadhalika. Katika makala ijayo, tutaangalia mambo muhimu kwenye uchunguzi wa Afya ya Mwanamke.
ASANTE SANA KUTEMBELEA BLOGU YETU..KARIBU TENA.
No comments:
Post a Comment