KWA jinsi maisha ya sasa yalivyo na pilikapilika nyingi za kujitafutia riziki, wakati mwingine hata mtu kupata muda wa kumuona daktari akiwa haumwi sana, mara nyingi inakuwa ni vigumu.
Hata hivyo mwili wa binadamu ni sawa na mashine inayofanya kazi nyingi, hivyo ili mwili huo uweze kufanya kazi vizuri, unahitaji matunzo, ikiwemo uchunguzi wa mara kwa mara wa kiafya ili kuhakikisha ubora na uimara wa mwili wenyewe.
Uchunguzi wa afya kwa ukawaida ni muhimu kwa wanawake wote bila kuzingatia umri hata kama huna dalili za ugonjwa wowote.
Makala haya ya Tabibu Wa kweli, kama mada inavyojieleza, yanahusu Mambo Muhimu ya Kufanyia Uchunguzi wa Kiafya kwa Mwanamke, pindi kina mama wanapotaka kufanyia uchunguzi wa afya ya mwili kiujumla.
Hayo ni pamoja na magonjwa ya klamidia, maambukizi ya VVU, moyo, kiwango cha kolesteroli, kisukari, utendaji wa viungo vikubwa vya mwili, osteoporosisi (aina ya kusinyaa kwa mifupa ya sehemu moja au mifupa yote miwili ambapo tishu ya mfupa hupotea lakini bila ya kuathiri muundo wa mfupa mzima) pamoja na saratani za aina mbalimbali, hasa zilizozoeleka kama vile saratani ya Ini, utumbo mpana na ya shingo ya kizazi.
Katika kufanyia uchunguzi maeneo hayo, Daktari huoanisha maelezo yanayotolewa na mtu anayefanyiwa uchunguzi kuhusu dalili zilizomsukuma kuhitaji kufanyiwa uchunguzi; historia yake ya nyuma kiafya; staili ya maisha, hasa ulaji wa vyakula; umri wa mhusika, historia ya familia yake kiafya; shughuli anazofanya na kama anatumia bidhaa za tumbaku kama vile sigara pamoja na unywaji wa pombe.
Wakati wa kuchunguza afya ya mwanamke daktari anaweza kumwomba mteja wake afunue baadhi ya maungo yake ya mwili au kuvua nguo kabisa ili kufanya uchunguzi vizuri. Vitu vinavyoweza kufanyika ni pamoja na kuchukua sampuli kwa pamba kutoka kwenye via vya uzazi au seviksi pamoja na kuchunguza sehemu za nje za via hiyo, sampuli ya mkojo na sampuli ya damu.
Aina ya vyakula vinavyotumiwa mara nyingi katika maisha ya siku hizi pamoja na aina ya mafuta yanayotumika kupikia vyakula, vinamuweka binadamu katika hatari ya ongezeko la kiwango cha kolesteroli kwenye damu, kinachoweza kusababisha magonjwa ya Moyo, hivyo ni muhimu kupima kiwango cha kolesteroli kama kiko katika hali ya kawaida au kimezidi. Klamidia ni ugonjwa wa zinaa unaosababishwa na bakteria waitwao kitalamu kwa jina la Klamidia, hivyo magonjwa haya yanapaswa kupimwa kwa kutumia kipimo cha Klamidia, ambacho wanawake wanaojali afya zao hufanyiwa uchunguzi walau mara moja kila mwaka kuanzia kipindi cha kuanza balehe.
Ni muhimu pia mwanamke anapofanyiwa uchunguzi wa afya ya mwili wake, akapima pia kama anaambukizi ya VVU pamoja na magonjwa mengine ya zinaa, kama vile kisonono, kaswende pamoja na virusi vya Human Papilloma Virusi (HPV). HPV ni ugonjwa wa zinaa ambao huwapata wanawake wengi zaidi ulimwenguni. Hasa nchi za ulimwengu wa tatu, Tanzania kiwemo. Chanzo kikuu cha ugonjwa huu ni saratani ya mlango wa tumbo la uzazi.
Kwa hiyo, inashauriwa mwanamke yeyote mwenye umri wa miaka 18 na kuendelea, kufanyiwa kipimo cha Pap (Pap Smear) kila baada ya miaka mitatu, ili kubaini mapema kama ana tatizo lolote katika mlango wa tumbo la uzazi. Hata hivyo, inashauriwa kwa wanawake wenye umri wa miaka 30 na kuendelea, kufanya kipimo hicho cha Pap pamoja na cha HPV kila baada ya miaka mitano. Mara nyingi, kipimo hicho cha Pap huhusisha uchunguzi wa chembe za seviksi (mlango wa tumbo la uzazi), ambazo huchukuliwa na madaktari kwa kutumia kijiko kidogo au brashi maalumu.
Ili kuchunguza sehemu za ndani za uzazi, Daktari anaingiza vidole vya mkono kwenye njia ya uzazi, huku mkono mkono mwingine akiwa ameshika tumbo ili kuhisi ovari au glandi za uzazi za mwanamke vinavyotoa yai pamoja na uterazi/kizazi (ogani ambamo utungo wa mimba hupokelewa na kustawishwa).
Endapo Daktari atahisi kitu kisicho cha kawaida kama vile uvimbe wa aina yoyote, atatoa ushauri wa vipimo gani vifanywe, kama vile Ultrasound, kwa ajili ya kubaini tatizo ili kuchukua hatua za matibabu mapema. Mwanamke anatakiwa pia kufanyiwa uchunguzi wa Matiti kwa kutumia Mamografi. Uchunguzi wa matiti kwa mamografi unahusisha X-ray ya tishu laini za matiti ili kuchunguza matiti kama yana uvimbe au saratani baada ya Daktari kuchunguza kwa njia ya kupapasa kwa mkono ili kuhisi uvimbe wowote.
Ikiwa kuna saratani yoyote iliyobinika, mgonjwa anaweza kushauriwa kukata titi/matiti ili kuzuia saratani kusambaa mwili mzima, la kama utakuwa ni uvimbe wa jipu tu, mgonjwa hukamliwa usaha na kupewa antibiotiki (kiuavijasumu).
Osteoporosisi ni ugonjwa wa kusinyaa kwa mifupa ya sehemu moja au mifupa yote ya miwili bila ya kuathiri muundo wa mfupa mzima. Mwanamke anapawa kufanya kipimo cha osteoporosisi walau mara moja kwa mwaka, hasa anapofikia umri wa kuanzia miaka 65. Huu ni ugonjwa ambao mtu anaweza kuupata kwa njia ya kurithi kutoka kwenye familia au akaupata kutokana na mwenendo wake wa maisha kama vile uvutaji wa sigara, kukoma kwa hedhi na kadhalika.
Aidha, mwanamke anashauriwa kufanyiwa uchunguzi wa Shinikizo la Damu kila mara anapotembelea kituo cha kutolea huduma za afya, hasa kwa kina mama wajawazito au kwa kina mama wenye umri wa zaidi ya miaka 35.
Viwango vya shinikizo la damu vinatofautiana kulingana na umri wa mwanamke pamoja na hali ya ujauzito. Kupima mara kwa mara kipimo cha shinikizo la damu, kunasaidia kufahamu kiwango cha kawaida na kisicho cha kawaida.

ASANTE SANA KUTEMBELEA BLOGU YETU KARIBU TENA.