Kansa ya matiti
ni aina ya kansa inayojitokeza toka tishu za matiti hasa mirija
myembamba inayopitisha maziwa. Ugonjwa huu (Saratani ya matiti) hutokea
kwa binadamu na mamalia wengine. Idadi ya wanaume wanaopatwa na kansa ya
matiti ni ndogo sana ikilinganishwa na ya wanawake.
Ulimwenguni pote, kansa ya matiti hubeba asilimia 29 nukta tisa ya kansa zote kwa wanawake.
Licha ya maendeleo ya kitiba, bado kansa ya matiti ndiyo kansa inayosababisha vifo vingi zaidi vya wanawake.
Nchi
zilizoendelea za Amerika Kaskazini na Ulaya Magharibi ndizo zenye idadi
kubwa zaidi ya watu walio na kansa, lakini idadi ya wanawake walio na
kansa ya matiti inaongezeka katika bara la Asia na Afrika ambako kwa
kawaida kumekuwa na idadi ndogo kiukweli.
Idadi ya
wanaokufa kati ya wale wanaogundulika kuwa na ugonjwa huo huko Asia na
Afrika ni ya juu kwasababu kansa hiyo haigunduliwi mapema. Wagonjwa
wengi huja ikiwa tayari imeenea sana.
Kansa ya matiti
huanza wakati ambapo chembe moja inajigawanya haraka sana isivyo
kawaida na bila utaratibu, na hatua kwa hatua inafanyiza uvimbe.
Uvimbe unakuwa
kansa wakati chembe zake zinapovamia tishu nyingine. Uvimbe fulani
unaweza kuchukua miaka kumi hivi kabla ya kugunduliwa.
VIHATARISHI/VISABABISHI
Hatari ya
kupatwa na kansa hiyo huongezeka dadiri umri unavyosonga. Asilimia 80
hivi ya wanawake wenye kansa ya matiti wana umri unaozidi miaka 50.
Lakini jambo linalofariji ni kwamba kansa ya matiti ni mojawapo ya kansa zinazoweza kutibiwa kwa urahisi.
Watakao tibiwa kabla ya kansa hiyo kuenea wanaweza kuishi muda mrefu kwa ukawaida.
Visababishi vya kansa ya matiti bado ni fumbo.
Baadhi ya
wanasayansi wanaamini kwamba kansa ya matiti hutokana na hatua nyingi
tata ambazo huanza wakati ambapo chembe fulani ya urithi yenye kasoro
inapofanya chembe zitende kwa njia isiyo ya kawaida, yaani, zigawanyike
kwa kasi sana, zishambulie tishu nyingine na kuepuka kuharibiwa na mfumo
wa kinga, kisha pole pole chembe hizo zinashambulia na kuharibu viungo
muhimu vya mwili.
Jambo lingine linalohusishwa na kansa ya matiti ni homoni ya estrojeni ambayo huenda inachochea aina fulani za kansa hiyo.
Kwa hiyo,
mwanamke anaweza kupatwa na kansa hiyo ikiwa alianza kupata hedhi mapema
maishani au ikiwa aliacha kupata hedhi akiwa amechelewa isivyo kawaida,
ikiwa alipata mimba ya kwanza umri wake ukiwa umesonga au ikiwa
hakuwahi kupata mimba, au ikiwa alipata matibabu ya kurudisha homoni
fulani mwilini.
Kwa kuwa chembe
za mafuta hutokeza estrojeni, huenda wanawake walionenepa kupita kiasi
waliofika umri wa kuacha kupata hedhi na hivyo ovari zao hazitokezi tena
homoni, wakawa katika hatari ya kupatwa na kansa hiyo.
Pia watu walio
na viwango vya juu vya insulini na watu walio na viwango vya chini vya
homoni ya usingizi inayoitwa melatonia kama vile watu wanaofanya kazi
usiku, wako pia katika hatari ya kupatwa na kansa hiyo.
Uvutaji wa
tumbaku umeonekana kuongeza hatari zaidi ya kupata saratani ya matiti,
kiwango kikubwa cha tumbaku iliyovutwa na kuanza kuvuta tumbaku katika
umri mdogo hufanya hatari kuongezeka zaidi.
Mionzi na
kemikali za viwandani huongeza hatari ya kansa ya matiti. Kemikali kama
polychlorinated biphenyls, polycyclic aromatic hydrocarbons na dawa za
kuulia wadudu huchangia kutokea saratani hiyo.
DALILI
– Uvimbe wowote au kuongezeka kwa unene wa ngozi kwenye makwapa au titi.
– Umajimaji wowote unaotoka kwenye chuchu ambao si maziwa.
– Mabadiriko yoyote ya rangi au ngozi ya titi.
– Chuchu iliyodidimia kwa njia isiyo ya kawaida au inayowasha.
UCHUNGUZI KUJUA KAMA NI KANSA
Ili kuchunguza ikiwa uvimbe una kansa sindano nyembamba hutumiwa kutoa tishu kutoka kwenye uvimbe huo na kufanyiwa uchunguzi.
MATIBABU
Uvimbe ukiwa na
kansa hufanyiwa upasuaji ili kuondoa uvimbe huo na tishu zinazozunguka
titi. Upasuaji husaidia kuonyesha uvimbe ulipofikia (ukubwa, aina na
kuenea kwake) na kuchunguza uvimbe unakua upesi kadiri gani.
Chembe zenye
kansa zinaweza kutoka kwenye uvimbe na kusafiri kupitia mfumo wa damu au
mfumo wa limfu na kuanza kukua tena mahali pengine mwilini.
Kuenea kwa
kansa hadi kwenye viungo na tishu muhimu kama vile ubongo, ini, uboho wa
mfupa au mapafu ndio hufanya ugonjwa huo uwe hatari.
Hivyo baada ya upasuaji, wagonjwa wengi hupata matibabu mengine ambayo yatazuia kansa isirudi na kuenea.
Kwasababu ya
maendeleo katika matibabu ya kansa ya matiti, kumekuwa na matibabu
mbalimbali ikitegemea umri, afya historia ya kansa katika familia, na
aina ya kansa.
Wanasayansi
wanajifunza mambo mengine kuhusu kansa kutia ndani kuelewa ni kwa nini
kansa huenea, kudhibiti chembe za kansa ambazo haziharibiwi kupitia
matibabu ya kemikali, kuzuia kugawanyika kwa chembe na kutibu kila
uvimbe kwa njia hususa.
No comments:
Post a Comment