Thursday, August 18, 2016

FAHAMU KILA KITU KUHUSU SARATANI YA DAMU (LEUKAEMIA).





Leukemia ni saratani inayoshambulia tishu za mwili zinazohusika na utengenezaji wa damu
zikiwemo supu ya mifupa (bone marrow) na mfumo wa lymph (lyphatic system). Kwa maneno rahisi, leukemia humaanisha saratani ya damu. Kuna aina mbalimbali za leukemia, nyingine zikiathiri watoto na nyingine zikiathiri zaidi watu wazima.

Kwa kawaida leukemia huanzia kwenye chembe nyeupe za damu yaaniwhite blood cells, ambapo mwili huzalisha kiwango kikubwa cha seli zenye maumbo mabaya ambazo hazina uwezo wa kufanya kazi zake sawasawa. Kazi ya chembe nyeupe za damu ni kulinda mwili dhidi ya vimelea waletao maradhi mbalimbali.

Leukemia husababishwa na nini?Kama zilizo kwa aina nyingi za saratani, mpaka sasa chanzo halisi cha leukemia hakijulikani. Hata hivyo, wanasayansi wanadai kuwa leukemia hutokea kutokana na mkusanyiko wa vyanzo mbalimbali vikiwemo vinavyohusu sababu za kinasaba (genetic factors) na kimazingira.

Kwa ujumla, leukemia hutokea pindi chembe nyeupe za damu zinapobadilika muundo wake wa kinasaba yaani viasili vyake vya DNA, ambavyo kwa kawaida hubeba maelekezo yanayoifanya seli yeyote ya kiumbe hai iweze kuishi, kutenda kazi zake, kujizaa na hata kufa, vinapobadilika maumbile na muundo wake kutokana na sababu mbalimbali. Kitendo cha kubadilika kwa maumbile na muundo wa DNA hujulikana kama mutation.

Ndiyo kusema basi, seli yeyote iliyopatwa na tatizo hili huwa na tabia ya kukua kwa haraka na kujizaa (kujigawa) kwa kasi zaidi kuliko kawaida, na pindi inapofikia muda wake wa kufa seli hiyo hugoma kufa badala yake huendelea kujizaa zaidi hatimaye kusambaa kwa wingi katika mfumo mzima wa damu, hali inayosababisha saratani ya damu.
               
Je, kuna vihatarishi vya leukemia?Ndiyo vipo! Pamoja na kwamba chanzo halisi cha saratani ya damu hakijulikani, lakini kuna mambo ambayo humuongezea mtu hatari ya kupata ugonjwa wa saratani ya damu.

Mambo ambayo yanaweza kuongeza uwezekano wa kupata saratani ya damu ni pamoja na:
Historia ya matibabu ya saratani hapo kabla: Watu ambao wamekuwa kuwa na aina nyingine za saratani hapo awali, na wakati wa matibabu wakapewa tiba ya mionzi au madawa makali ya saratani, wapo katika hatari kubwa ya kupata saratani ya damu kwa sababu baadhi ya dawa hizi pamoja na mionzi huwa na tabia ya kuathiri pia seli nyeupe za damu pamoja na tishu zinazotengeneza seli hizo.
Kuwa na magonjwa mengine ya vinasaba:

Ingawa haieleweki sawasawa uhusiano wake ulivyo, kuwa na baadhi ya magonjwa ya kinasaba kama vile ugonjwa wa Down syndrome, yasemekana huongeza uwezekano wa muathirika kuugua pia ugonjwa wa saratani ya damu.

Baadhi ya magonjwa mengine ya damu: 
Watu wenye magonjwa mengine ya damu kama vile ugonjwa wa damu unaoshambulia tishu za supu ya mifupa na kuzifanya zizalishe seli nyingi za damu bila uwiano unaotakiwa yaanimyelodysplastic syndromes, huongeza pia uwezekano wa mtu kuugua saratani ya damu.

Kupigwa na kiasi kikubwa cha mionzi: 
Watu ambao wamewahi kupigwa na kiasi kikubwa cha mionzi kama vile mlipuko wa mabomu au kulipuka kwa vinu na mitambo ya nuklea (nuclear reactors), wana hatari kubwa zaidi ya kupata saratani ya damu pamoja na saratani nyingine.

Kupigwa/kutumia baadhi ya kemikali:
Watu waliowahi kukumbana na baadhi ya kemikali kama vile benzene au zile zinazotumika kwenye viwanda vya kuyeyusha vyuma au kutengeneza magurudumu au mabomba ya plastic, nao pia wapo katika uwezekano mkubwa wa kupata saratani ya damu.

Uvutaji sigara: 
Jambo hili pia huongeza uwezekano wa kupata aina mojawapo ya saratani ya damu.
Kuwa na historia ya ugonjwa huu katika familia:

 Watu ambao, baadhi ya ndugu zao wamewahi kuugua ugonjwa huu, nao pia wana uwezekano mkubwa wa kupata saratani ya damu. Hata hivyo, hii haina maana kwamba leukemia inaambukizwa isipokuwa kuna uhusiano wa kifamilia tu katika kusababisha ugonjwa huu.

Jambo moja la kufahamu ni kuwa, wapo watu wengi ambao wamewahi kukumbana na vihatarishi nilivyovieleza hapo juu bila kupata leukemia, kadhalika wapo waliopata leukemia bila kukumbana na kihatarishi hata kimoja kati ya hivi. Kwahiyo. Uwepo wa vihatarishi hivi haimaanishi kuwa ni lazima mtu apate leukemia isipokuwa inaongeza uwezekano wa kupata ugonjwa huu.
                                                      
Makundi ya leukemiaWataalamu wa afya wanaiainisha leukemia katika makundi mbalimbali kulingana na kasi ya kusambaa kwa ugonjwa pamoja na aina ya chembe damu zilizoathirika.
Kulingana na aina ya chembe damu zilizoathirika, leukemia inaweza kugawanywa katika makundi makuu mawili, ambayo ni:

Leukemia inayoathiri zaidi chembe damu zinazounda mfumo wa lymph ambayo kwa kitaalamu huitwa Lymphocytic leukemia. Mfumo wa lymph au lymphatic system ndiyo unaolinda mwili wako dhidi ya maradhi na maambukizi mbalimbali kama vile VVU n.k. Chembe damu zinazohusika hapa huitwa lymphocytes.




Leukemia inayoathiri zaidi chembe/seli zinazounda chembe damu nyingine za mwili yaani kwa kitaalamu Myelogenous leukemia. Aina hii ya leukemia huathiri chembe zinazoitwamyeloid cells, ambazo ndizo huzaa chembe nyekundu za damu, chembe nyeupe za damu pamoja na chembe sahani. Chembe nyekundu husaidia kusafirisha hewa safi ya oksijeni mwilini na kutoa hewa chafu ya kabondioksaidi, chembe nyeupe hupambana na vimelea wa magonjwa mbalimbali kama vile uti wa mgongo, minyoo, kifua kikuu, nk., wakati chembe sahani husaidia kuganda kwa damu pindi mtu unapoumia au kujikata.

Njia ya pili ya kuainisha makundi ya leukemia ni kwa kuangalia kasi ya kusambaa kwa ugonjwa wa saratani ya damu mwilini mwa muathirika. Kwa njia hii, kuna makundi makuu mawili ya leukemia, ambayo ni:

Leukemia inayosambaa kwa haraka au wataalamu wanaitaacute leukemia. Katika aina hii, chembe damu huwa changa, zenye mambo mabaya yasiyo ya kawaida, na zisizoweza kufanya kazi zao vizuri. Lakini mbaya zaidi, hujigawa na kuzaliana kwa kasi kubwa kiasi cha kusambaa na kujazana katika damu kwa muda mfupi sana.

Leukemia inayosambaa taratibu au kwa kitabibu chronic leukemia. Katika aina hii, chembe damu huwa zimekomaa na zenye uwezo wa kujigawa na kuzaliana taratibu na hata kufanya kazi zake kama kawaida. Chembe damu huweza kuishi kwa muda mrefu bila hata mgonjwa kuonesha dalili yeyote ya kuugua leukemia.

Aina za Leukemia 
Bila kujalisha kasi ya kusambaa kwa ugonjwa au aina ya chembe damu iliyoathirika, leukemia inaweza kugawanywa katika aina zifuatazo:

Leukemia inayosambaa kwa haraka huku ikishambulia chembe damu zinazounda mfumo wa lymph yaani Acute lymphocytic leukemia (ALL). Aina hii huwapata zaidi watoto wenye umri mkubwa kidogo ingawa pia inaweza kwa kiasi fulani kuwapata hata watu wazima.

Leukemia inayosambaa kwa haraka huku ikishambulia chembe/seli zinazounda chembe damu nyingine za mwili yaaniAcute myelogenous leukemia (AML). Aina hii ya leukemia inaongoza kati aina nyingine zote na huwapata watoto pamoja na watu wazima.

Leukemia inayosambaa taratibu huku ikishambulia chembe damu zinazounda mfumo wa lymph yaani chronic lymphocytic leukemia (CLL). Aina hii huwapata zaidi watu wazima, na nadra sana kutokea kwa watoto. Wagonjwa wa aina hii ya leukemia huweza kuishi vizuri kabisa bila kuwa na dalili zozote zile.

Leukemia inayosambaa taratibu huku ikishambulia chembe/seli zinazounda chembe damu nyingine za mwili yaanichronic myelogenous leukemia (CML). Watu wazima ndiyo waathirika wakubwa zaidi wa aina hii ya saratani ya damu. Mtu mwenye aina hii ya leukemia anaweza akapata dalili chache au asiwe na dalili kabisa kwa miezi hata miaka kabla ya ugonjwa kufumuka ghafla na kuanza kumshambulia.

Dalili za leukemia ni zipi?
Dalili za leukemia hutofautiana kutoka aina moja mpaka nyingine. Hata hivyo, dalili za jumla za leukemia ni pamoja na;

  1. Homa au kujihisi baridi
  2. Uchovu na ulegevu wa mwili
  3. Maambukizi ya mara kwa mara
  4. Kupoteza uzito bila kukusudia
  5. Kuvimba tezi za mitoki
  6. Kuvimba wengu (splenomegaly)
  7. Kuvimba ini (hepatomegaly)
  8. Kutokwa damu kirahisi na kupata michubuko ya mara kwa mara
  9. Kuvilia kwa damu chini ya ngozi
  10. Kutokwa jasho kupita kiasi hasa nyakati za usiku
  11. Kuhisi maumivu ya mifupa
  12. Kupungukiwa damu mara kwa mara

Mara nyingi dalili za Leukemia hazipo wazi na ni rahisi sana kwa mgonjwa kuchanganya na dalili za magonjwa mengine, hivyo ni vema kuwahi hospitali kwa ajili ya uchunguzi wa kina na vipimo, mara tu uonapo dalili zilizotajwa hapo juu.

Uchunguzi na vipimoNi rahisi kwa daktari kugundua leukemia inayosambaa kwa kasi (acute leukemia) kuliko ile inayosambaa taratibu (chronic leukemia). Mara nyingi leukemia inayosambaa taratibu hugunduliwa mgonjwa anapoenda hospitali kwa ajili ya matibabu ya kitu kingine tofauti.

Pamoja na kukuuliza historia yako kwa lengo la kufahamu dalili na vihatarishi vya ugonjwa huu, daktari pia atakufanyia uchunguzi wa kina wa mwili kwa ajili ya kuchunguza uwepo wa viashiria vya saratani ya damu kama vile ngozi nyeupe (katika viganja, macho au ulimi), kuvimba kwa tezi za mitoki, kuvimba wengu na ini; kuvilia damu katika ngozi, michubuko, au kama una dalili zozote za upungufu wa damu mwilini.

Vipimo 
utakavyofanyiwa ni pamoja na
Kipimo cha damu almaarufu kama Full Blood Picture ambacho huonesha kiwango cha kila chembe damu iliyopo mwilini. FBP huonesha kama chembe damu nyeupe zimeongezeka ama la, sambamba na chembe damu nyingine. Pia huonesha kiasi cha wingi wa damu, na iwapo mgonjwa ana upungufu wa damu ama la. Kwa ujumla wagonjwa wa leukemia huwa na ongezeko kubwa la chembe damu nyeupe zilizo changa, wakati chembe damu nyekundu pamoja na chembe sahani huwa chini.

Kipimo cha supu ya mifupa (bone marrow biopsy) hufanyika kwa ajili ya kuchunguza uwepo wa seli za saratani. Kipimo hiki hufanyika kwa kuchukua sehemu ya mfupa wa nyonga au paja, kisha kuepelekwa maabara kwa uchunguzi. Biopsy husaidia kutofautisha kati ya leukemia na magonjwa mengine ambayo husababisha kuwepo kwa ongezeko la chembe damu nyeupe. Kwa maneno mengine, hiki ni kipimo tosha cha uthibitisho wa kuwepo kwa leukemia.

Vipimo vingine ni pamoja na vile vinavyoonesha utendaji kazi wa figo (renal function tests) na ini (liver function tests).
Baadhi ya madaktari hupenda pia kufanya kipimo cha uti wa mgongo (lumbar puncture) ili kuchunguza uwepo wa chembe za leukemia katika maji ya uti wa mgongo (spinal fluid).

Matibabu
Matibabu ya leukemia hutegemea mambo mbalimbali kama vile hatua ugonjwa ulipofikia, umri wa mgonjwa, hali ya jumla ya kiafya ya mgonjwa, na aina ya leukemia.
Leukemia inaweza kutibiwa kwa kutumia:

Dawa za kuua seli za saratani (chemotherapy): Hii ni njia kuu ya matibabu ya leukemia, ambapo dawa hutumika kuua seli zenye saratani. Kutegemeana na aina na hatua iliyofikiwa na ugonjwa, mgonjwa anaweza kupewa dawa moja au mkusanyiko wa dawa kadhaa tofauti tofauti kwa muda fulani.
Tiba ya mionzi (radiotherapy):

Njia hii hutumia mionzi yenye nguvu kubwa iliyoelekezwa kwa ajili ya kuua chembe za leukemia na kuzuia ukuaji wake. Mionzi inaweza kutolewa katika eneo fulani maalum la mwili ambapo kuna kusanyiko la chembe za leukemia au mwili mzima.

Dawa zinazoelekezwa mahsusi kuua viasili vya seli za saratani (targeted therapy): Dawa hizi hufanya kazi maalum ya kuzuia seli kuzaliana au kujigawa kwa kuingilia mfumo wake wa utendaji kazi.
Tiba ya upandikizaji (stem cell transplant):

Tiba hii hufanyika kwa ajili ya kurejesha sehemu ya supu ya mfupa iliyoharibika kwa kuweka supu mpya. Kabla ya tiba hii, mgonjwa hupewa dawa za kuua seli za saratani au mionzi ili kuua kabisa eneo lililoathiriwa kisha supu mpya hupandikizwa. Mara nyingi supu hii hutoka kwa mtu mwingine (donor) au inaweza ikatoka kwa mgonjwa mwenyewe kwa kuchukua sehemu ambayo haijaathirika.

Na njia nyingine ni tiba ya kuchochea mfumo wa kinga ya mwili kuzitambua, kushambulia na hatimaye kuua seli za saratani (biological therapy).

Nini cha kufanya?Saratani ya damu ni jambo la kutisha na kusikitisha hususani kwa familia ambayo inamuhudumia mgonjwa wa tatizo hilo. Aidha ni jambo la kuhuzunisha sana kwa wazazi wenye mtoto aliyegunduliwa kuwa na ugonjwa huu.

 Kwa familia iliyokumbana na tatizo hili ni vema kufahamu nini cha kutarajia na kufanya. Kwa mzazi, hana budi kutafuta taarifa zaidi ya ugonjwa wa mtoto wake, aina ya ugonjwa, hatua iliyofikia na aina za matibabu yanayomfaa mtoto wake. Kwa mgonjwa, ni vema kufuatilia ushauri wa wataalamu wa afya na kuwa makini katika kutoa taarifa ya mabadiliko yeyote unayoyaona kuhusu maendeleo ya afya yako.

Kwa jamii nzima, ni muhimu kujiepusha na vihatarishi vinavyoweza kuongeza uwezekano mtu kupata saratani ya damu.


ASANTE SANA KUTEMBELEA BLOGU YETU...KARIBU TENA.

   Dr Theobard M.Rwiza.

No comments:

Post a Comment