Sunday, August 21, 2016

ELEWA NI JINSI GANI YA KUMSAIDIA MTOTO MWENYE MTINDIO WA UBONGO.



KATIKA hali ya kawaida baadhi ya watoto wanaweza kuzaliwa wakiwa na matatizo mbalimbali yanayoweza kusababishwa na sababu mbalimbali.

Katika makala ya leo tuangalie tatizo la mtindio wa ubongo kwa watoto. Tatizo hili linatokana au linasababishwa na vinasaba (Genetic), anavyokuwa ametumia mama wakati wa ujauzito.

Miongoni mwake ni pamoja na dawa za kulevya, pombe, hali ya dawa alizotumia mama wakati wa ujauzito, matumizi ya madawa ya kulevya, pombe, hali ya hewa, au hata ajali.

Kati ya sababu zinazotajwa zinaweza kusababisha mtoto kuzaliwa akiwa na mtindio wa ubongo au kupatwa na tatizo hilo akiwa ameisha zaliwa.

Kwa upande wa pombe inakuwa na athari kubwa na mbaya kwa mama mjamzito. Kwa mama mjamzito  anayetumia kiasi kikubwa cha pombe akiwa mjamzito pia mtoto wake anaweza kupata tatizo linalojulikana kitaalamu kama Fetal Alcoholic Syndrome (FAS).

Baadhi ya wanawake wamekuwa na kawaida ya kutumia dawa za aina mbalimbali pindi wanapokuwa wajawazito bila kupata ushauri wa kitaalamu jambo linalochangia mtoto kuzaliwa na tatizo hilo. Hii inamuathiri mtoto hasa katika miezi ya mwanzo ya kutungwa kwa mimba.

Kutokana na hali hiyo unywaji wa pombe hata kwa kiwango kidogo katika kipindi cha mwezi mmoja hadi mitatu ya mwanzo kwa mama mjamzito huchangia kwa kiasi kikubwa kuzaliwa kwa watoto wenye matatizo haya.

Watoto wanaozaliwa na tatizo hili wanakuwa na nyuso ambazo sio za kawaida (Facial Deformities), kwa mfano watoto hawa wanaweza kuwa na pua bapa na macho yaliyoingia ndani au kuwa na mtindio wa ubongo (Mental Retardations), matatizo ya kusikia na kutokuwa na uwezo wa kusoma.

Watoto wote wenye matatizo haya ya mtindio wa ubongo wanaweza pia kujifunza kusoma iwapo watapewa msaada maalum na kuandaliwa mazingira mazuri yatakayowashawishi kujifunza kusoma.

Malezi kwa watoto wenye matatizo haya, yanatakiwa yawe tofauti na yale ya watoto wa kawaida.

Watoto hawa wanahitaji kuoneshwa upendo, kusikilizwa na mengineyo ya aina hiyo ingawa inaweza kuwepo changamoto ya bkutambua watoto wenye tatizo hilo wakiwa wadogo.

Huwa vigumu mzazi au jamii kumtambua mtoto mwenye tatizo la mtindio wa ubongo hasa akiwa na umri chini ya miaka minne. Kutokana na hali hiyo ya ugumu wa kutambua mtoto mwenye tatizo hilo mapema wataalamu wa afya hushauri mtoto yeyote ambaye anafanya mambo yake pole pole ukilinganisha na watoto wengine wa umri wake, inapaswa kupelekwa haraka hospitalini kwa daktari bingwa wa watoto ili afanyiwe uchunguzi wa kina.

Licha ya hiyo baadhi ya dalili inazoweza kumsaidia mzazi kugundua tatizo la mtoto wake ni pamoja na mtoto kutolia, kulia kwa kiasi kidogo , kuchelewa kutembea pamoja na kutochangamaka ukimlinganisha na watoto wenye rika kama la kwake.

Pia mtoto huyo anaweza kuonyesha kutovutiwa na mazingira yanayomzunguka, kwa maana kwamba hata kama kuna vitu vya kuchezea hawezi kujishughulisha navyo.

Aidha huwa ngumu sana mtoto mwenye tatizo hilo kufundishika ikiwemo kusoma na kufanya shughuli nyingine zinazowahusu watoto.

Mtoto huyo hawezi kula peke yake , kuvaa mwenyewe au kujifunza kutumia choo. Hata hivyo zipo dalili nyingi zinazoweza kujitokeza na mara nyingi zinatambuliwa na madaktari maalum wa watoto.

Jinsi ya kumsaidia mtoto mwenye tatizo hilo


Mtoto mwenye mtindio wa ubongo anafundishika, iwapo tu atafundishwa kwa makini, utulivu na uvumilivu mkubwa, yaani mtu anayemfundisha mtoto wa aina hii haitakiwi kamwe kuwa na hasira, na pia inashauriwa sana kuwapongeza wanapofanya vizuri japo kidogo.

Kama ni mwalimu anatakiwa awe mpole na ufundishaji wake usiwe wa haraka haraka, aoneshe mapenzi kwa mtoto.

Watoto wa aina hii inashauriwa wapewe nafasi ya kujenga urafiki na watoto wenzao warika lao ili weweze kujifunza baadhi ya mambo yanayowezekana kulingana na uwezo wao wa kujifunza.

Iwapo mtoto mwenye ugonjwa huu atatengwa na wenzake hali hiyo itamsababishia kutokuwana maendeleo yoyote ya kuweza kufanya jambo lololte ukilinganisha na yule mwenye tatizo kama lake lakini amepata nafasi ya kuchanganywa na wenzake.

Licha ya wataalamu kushauri watoto hao wachganganywe na wenzao lakini pia jamii imekuwa na kawaida ya kuwatenga na kuwababgua watoto hao bila kujali kuwa nao wanahitaji haki kama walivyo watoto wasio na ulemavu huo.

Maranyingi mtoto mwenye tatizo hili anaweza kupata msaada wa mazoezi ya viungo na mazoezi mengine mepesi yatakayomsaidia kuendelea na maisha kama walivyo watoto wengine.

Ushauri.


Wazazi wanashauriwa pale wanapozaa mtoto mwenye tatizo hili kumchukulia kuwa ni mtoto kama walivyo watoto wengine ili kuiwezesha jamii inayomzunguka kumchukulia kawaida na endapo wataonyesha dalili za kumtenga hata jamii hiyo pia itaweza kumtenga na kumnyanyapaa.

Wazazi wanatakiwa kuonyesha ushirikiano na kuonyesha upendo kwa mtoto huyo na  sio kumtenga kama ilivyo kwa wazazi wengine wanaofikia hatua ya kufarakana kutokana na kuzaa mtoto mwenye ulemavu wa aina hii.

Baadhi yao wamekuwa wakifikia hatua ya kumtelekeza mtoto wao jambo ambalo ni kinyumbe hata na sheria za kibinadamu.

Licha ya mtoto huyo kuonyeshwa upendo na wazazi pamoja na jamii inayomzunguka pia wanatakiwa kuzingatia mazoezi ya viungo  na ushaur wanaokuwa wamepewa na wataalamu wa afya.


ASANTE SANA KUTEMBELEA BLOGU YETU...KARIBU TENA.

  Dr Theobard M.Rwiza.

No comments:

Post a Comment