Katika hatua zote za makuzi ya binadamu wa kawaida, kuna mabadiliko ya kimwili ambayo hutokea tangu utotoni mpaka uzeeni. Ni mabadiliko ya urefu na uzito.
Na katika kila hatua, uwiano uliopo kati ya uzito na urefu wa miili yetu ni kipimo tosha cha kuonyesha kama uzito wetu hauna madhara kwa afya zetu au kinyume chake. Kwa Kiingereza uwiano huu unaitwa “Body Mass Index” au BMI kwa kifupi.
Kipimo cha BMI hutumika kutathimini hali ya lishe zetu, ikiwa ni pamoja na watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (VVU). Pia, kipimo cha BMI hutusaidia kugundua mapema baadhi ya matatizo ya afya na lishe na hivyo kuwasaidia watoa huduma za afya kuweza kutoa ushauri ipasavyo kwa wateja wao.
Katika makala hii FikraPevu inakufahamisha jinsi ya kutafuta na kutafsiri kipimo cha MBI kwa makundi mbalimbali ya watu.
Jinsi ya kutafuta kipimo cha BMI
Kipimo cha BMI hupatikana kwa kutafuta uzito, kutafuta urefu, na hatimaye, kugawanya uzito dhidi ya kipeuo cha pili cha urefu wa mhusika. Katika mchakato huu, uzito hupimwa katika kizio cha kilogramu na urefu kupimwa katika kizio cha mita. Kwa hiyo, kizio cha uwiano wa BMI ni “kilogramu kadhaa kwa kila meta moja ya eneo.”
Kwa mfano, tutatafuta BMI ya mtu mwenye kilo 62 na urefu wa sentimeta 160. Katika hatua ya kwanza tunapaswa kubadili sentimeta kuwa mita, kwa kuzingatia kwamba mita moja ni sawa na sentimeta 100. Yaani, sentimeta 160 ni sawa na meta 1.6 tu.
Katika hatua ya pili, tunatafuta kipeuo cha pilicha meta 1.6, ambacho ni 1.6 mara 1.6, sawa na meta za mraba 1.96. Na katika hatua ya tatu, tunagawanya uzito wa kilo 62 dhidi ya meta za mraba 1.96, na kupata kilogramu 24 kwa kila meta moja ya eneo.
Jinsi ya Kupima Uzito
Ili kupima uzito vizuri, tuhakikishe mshale wa mizani uko kwenye sifuri kabla ya kuchukua kipimo. Mtu anayepimwa anatakiwa kuvaa nguo nyepesi na kuvua viatu wakati wa kupimwa uzito. Mtu huyo anatakiwa kusimama wima katikati ya mizani bila kushikiliwa au kushikilia kitu chochote. Uzito urekodiwe katika kadirio la karibu la desimali moja. Kwa mfano, kilo 36.12 irekodiwe kilo 36.1 tu.
Jinsi ya Kupima kimo au urefu
Kusudi tupime uzito vizuri, mtu anayepimwa anatakiwa kuvua viatu, kusimama wima, kuangalia mbele huku miguu ikiwa pamoja na magoti yakiwa yamenyooka. Visigino, matako, mabega na mgongo vinatakiwa kugusa ukuta. Kisha, urefu urekodiwe katika kadirio la karibu la nusu sentimeta mfano sentimeta 120.53, urekodiwe kama sentimeta 120.5 pekee.
Jinsi ya kutafsiri matokeo ya kipimo cha BMI
Kwa watu wazima uwiano wa BMI ni kipimo cha kujua kama uzito wao unaendana na kimo chao. Kwa Watoto wa umri wa miaka miwili na zaidi, mfumo wa “BMI sentaili” (BMI Centile) hutumika. Hiki ni kipimo cha kujua kama uzito wa mtoto unaendana na kimo, umri na jinsia.
Mtu akiwa na BMI inayozidi mipaka yupo katika hatari zaidi ya matatizo ya kiafya kama vile kisukari, magonjwa ya moyo au saratani za aina tofauti tofauti.
Kwa mfano, kwa watu wenye umri wa miaka 20 au zaidi,  uwiano wa BMI unatafsiriwa kama ifuatavyo:
Uwiano wa BMI ulio chini ya kiwango cha 18.5 unamaanisha “uzito uko chini ya kiwango,” kati ya 18.5 na 24.9 unamaanisha “uzito ni wa wastani.”
Uwiano ulio kati ya 25.0 na 29.9 unamaanisha “uzito wa kuelekea kwenye kitambi.” Huonyesha tumezidi mipaka ya kawaida, yaani uzito wetu umezidi kawaida (OverWeight). Pia, ina maanisha wewe ni mzito zaidi kuliko mtu mwenye afya njema wa kimo chako.
Na kipimo cha BMI ya 30 na zaidi kinatafsiriwa kama uzito kupita kiasi au kiriba tumbo (obesity).
Kuwa na uzito kupita kiasi kunatuweka katika hatari zaidi ya matatizo ya kiafya kama magonjwa ya moyo, kiharusi (stroke) na kisukari.
Hata hivyo, baadhi ya watu wazima wana maumbo makubwa yanayoweza kusababisha BMI iwe juu zaidi ya mipaka hii. Mfano ni wachezaji wa Raga (Rugby) na mpira wa kikapu ambao wanaweza kuwa na Uzito uliozidi sana (Obese BMI) ingawa wana miili ya kawaida.
Uhusiano wa BMI, kipimo cha nyonga na magonjwa
Ni muhimu kufahamu kwamba, mtu mzima anaweza akawa na BMI nzuri lakini bado akawa na mafuta mengi kuzunguka tumbo lake. Jambo hili linaweza kumwongezea hatari ya kupatwa na magonjwa ya moyo, kisukari na kiharusi (stroke). Hivyo, utamaduni wa kupima ukubwa wa kiuno ni njia nzuri ya kuangalia kama mtu ana mafuta ya ziada kuzunguka tumbo lake. Ili kupima kiuno fuata utaratibu ufuatao:
Tafuta mbavu ya mwisho na juu ya nyonga na zungusha futi yako katikati ya mbavu ya mwisho na nyonga. Toa pumzi nje kabla ya kupima, na hatimaye chukua kipimo.
Bila kujali kimo au kipimo cha BMI tunapaswa kupunguza uzito ikiwa viuno vyetu ni sentimeta 94 au zaidi kwa wanaume, au sentimeta 80 au zaidi kwa wanawake. Na kwa ujumla, tunapaswa kuchukua hatua za kupunguza uzito iwapo BMI zetu ziko chini ya 18.5. Kupunguza uzito kuna faida nyingi kama vile kuimarika kwa afya, kuondoa maumivu ya mgongo na viungo.
Mbinu kubwa za kupunguza Uzito ni kupunguza vyakula vya wanga na mafuta, kufanya mazoezi ya mwili na wakati mwingine matumizi ya dawa. Kiwango cha mazoezi ya mwili huendana na umri.
Watu wazima wa kati ya umri wa miaka 18 hadi 64 wanapaswa kufanya mazoezi kwa angalau dakika 150 kwa siku, mazoezi kama kutembea kwa haraka na kuendesha baiskeli.
Kwa watu wazima wenye Uzito uliozidi kiasi wanapaswa kufanya zaidi ya mazoezi ya kutembea kwa haraka na kuendesha baiskeli.
Kutafuta kipimo cha BMI kwa kutumia chati ya kimo na uzito
Mbali na kutumia kanuni za mahesabu katika kutafuta vipimo vya BMI, bado tunaweza pia kutumia chati ya kimo na uzito (height and weight chart) kwa ajili hii. Tuone jambo hili kwa kuangalia vipimo vya BMI kwa watoto.
Baada ya kukokotoa “BMI Centile,” mtoto huanguka kwenye moja kati ya makundi manne yafuatayo:-
Kundi la chini ya uzito (UnderWeight): Hapa mtoto anakuwa chini ya BMI Centile ya Pili (Below second BMI Centile). Kundi la uzito mzuri kiafya (Healthy Weight): Hapa mtoto anakuwa kati ya BMI Centile ya Pili na BMI Centile ya Tisini (Between the second and ninetieth BMI Centile).
Kundi la uzito uliozidi (OverWeight): Hapa mtoto anakuwa kati ya BMI Centile ya Tisini na Moja na Tisini na Saba (Between ninety first to ninety seventh BMI Centile). Kundi la uzito kuzidi kiasi (Very OverWeight): Hapa mtoto anakuwa kati ya BMI Centile ya Tisini na Nane na zaidi.
Kwa ujumla, kama mtoto wako ana uzito uliozidi kiasi (Obesity) atakuwa katika hatari ya kubwa ya kuugua sana kipindi chake cha utoto hata katika maisha ya baadaye.

ASANTE KUTEMBELEA BLOGU YETU...KARIBU TENA.